Rais wa Iran awasili Beijing, kusaini hati 20 za makubaliano na China
(last modified Tue, 14 Feb 2023 02:59:43 GMT )
Feb 14, 2023 02:59 UTC
  • Rais wa Iran awasili Beijing, kusaini hati 20 za makubaliano na China

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amewasili Beijing, mji mkuu wa China kwa ziara rasmi ya kikazi, kufuatia mwaliko wa Rais Xi Jinping wa nchi hiyo.

Rais Sayyid Ebrahim Raisi wa Iran amewasili China alfajiri ya leo na kupokewa katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Beijing na Waziri wa Utamaduni na Utalii wa nchi hiyo ya Asia. Hii ni ziara rasmi ya kwanza ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini China baada ya kupita miaka 20.

Akiongea na waandishi wa habari katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mehrabad hapa jijini Tehran hiyo jana kabla ya kuondoka, Rais Raisi alisema Iran na China zitatiliana saini hati 20 za ushirikiano.

Ikumbukwe kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na China mwezi Machi mwaka 2021 zilitia saini mkataba wa ushirikiano wa miaka 25.

Sayyid Ebrahim Raisi ameashiria misimamo inayofanana ya Iran na China katika kupambana na ubeberu na kueleza kuwa, nchi mbili hizi zinapinga kwa dhati hatua za kujitanua na za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja na kusisitiza ulazima wa kuheshimiwa haki na maslahi ya nchi zote. 

Rais wa Iran akiondoka nchini kuelekea China

Kabla ya kuondoka nchini, Rais Raisi alisema serikali za Iran na China ambazo zimechagua Mpango wa Ushirikiano wa Pamoja wa Kimkakati kama kigezo cha mahusiano endelevu kati ya pande mbili, zina masuala mbalimbali ya pamoja na yale yenye kushabihiana kuhusu matukio ya kimataifa. 

Rais Raisi wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu na China ni wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Shanghai (SCO), na jukwaa hilo limezisaidia nchi mbilizi hizi kuwa na uhusiano wa karibu na nchi za Asia na maeneo mengine duniani.

Baadaye hii leo, Rais wa Iran anatazamiwa kupokewa rasmi na kufanya mazungumzo ya faragha na mwenzake wa China, Xi Jinping, kabla ya kufanyika mazungumzo ya wajumbe wa ngazi za juu wa nchi hizo mbili; pamoja na hafla ya kutiliana saini hati za ushirikiano ambayo itafanyika mbele ya marais hao mawili.