IRGC: Hakuna dola linaloweza kuchukua hatua dhidi ya Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i94042-irgc_hakuna_dola_linaloweza_kuchukua_hatua_dhidi_ya_iran
Msemaji wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC) ameashiria uwezo mkubwa wa kujihami wa Iran na kusisitiza kuwa, hakuna dola katika madola yenye nguvu duniani linaloweza kuchukua hatua za kichokozi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
Feb 14, 2023 04:36 UTC
  • IRGC: Hakuna dola linaloweza kuchukua hatua dhidi ya Iran

Msemaji wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC) ameashiria uwezo mkubwa wa kujihami wa Iran na kusisitiza kuwa, hakuna dola katika madola yenye nguvu duniani linaloweza kuchukua hatua za kichokozi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Brigedia Jenerali Ramezan Sharif amesema hayo katika hafla ya kuadhimisha miaka 44 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu katika mkoa wa Kerman, kusini mashariki mwa Tehran na kubainisha kuwa, hakuna adui anayeweza kuthubutu kufanya chokochoko dhidi ya Iran kwa kuwa wanafahamu fika uwezo mkubwa wa kijeshi na kiulinzi wa Iran.

Amesema, "Kwa Rehema za Allah, miongozo ya busara ya Kiongozi Muadhamu (wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei), na kujitolea muda wote vijana wetu, tumefikia kiwango cha uwezo wa kiulinzi na kijeshi kadri kwamba, Wamarekani na madola yoyote mengine hayajasiri kuchukua hatua japo ndogo ghalati dhidi ya nchi hii, taifa hili na maslahi yake."

Msemaji wa jeshi la SEPAH la Iran ya Kiislamu ameeleza bayana kuwa, vikosi vya Jamhuri ya Kiislamu vitasambaratisha usalama wa yeyote atakayejaribu kudhuru usalama wa taifa hili.

Makombora ya Iran

Brigedia Jenerali Sharif ameeleza bayana kuwa, tangu baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, watawala wa madola ya kibeberu na kiistikbari wakiongozwa na Marekani wamekuwa wakitekeleza uadui dhidi ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Msemaji wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran amesisitiza kuwa, pamoja na kuwepo njama hizo, lakini mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran una mizizi imara.

Kadhalika Brigedia Jenerali Ramezan Sharif amewapongeza wananchi wa Iran kwa kuwa macho, kuwa na maono na mtazamo wa mbali na busara, mkabala wa njama hizo za maadui.