Kan'ani: Kimya cha Magharibi mbele ya jinai za Wazayuni kinatia kichefuchefu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i94234-kan'ani_kimya_cha_magharibi_mbele_ya_jinai_za_wazayuni_kinatia_kichefuchefu
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani jinai za utawala wa Kizayuni katika viunga vya mji mkuu wa Syria, Damascus na kusema kuwa, kimya cha nchi za Magharibi kwa jinai na uvunjaji huo wa wazi wa haki ya kujitawala nchi mwanachama wa Umoja wa Mataifa, ni aibu na kinatia kichefuchefu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 19, 2023 08:24 UTC
  • Kan'ani: Kimya cha Magharibi mbele ya jinai za Wazayuni kinatia kichefuchefu

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani jinai za utawala wa Kizayuni katika viunga vya mji mkuu wa Syria, Damascus na kusema kuwa, kimya cha nchi za Magharibi kwa jinai na uvunjaji huo wa wazi wa haki ya kujitawala nchi mwanachama wa Umoja wa Mataifa, ni aibu na kinatia kichefuchefu.

Mapema leo alfajiri, ndege za utawala wa Kizayuni zimeingia kinyume cha sheria kwenye anga ya Syria na kufanya mashambulio katika baadhi ya maeneo ya kusini mwa nchi hiyo ya Kiarabu.

Ndege hizo zimeshambuliwa kituo cha rada kaskazini mwa mkoa wa as Suwaida wa kusini magharibi mwa Syria kama ambavyo zimeshambulia pia nyumba moja ya makazi ya raia, shambulio ambalo limepelekea watu wasiopungua 20 kuuawa na kujeruhiwa.

Shirika la habari la IRNA limemnukuu Nasser Kan'ani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran akigusia mashambulio ya mara kwa mara ya Wazayuni nchini Syria sambamba na mashambulizi ya genge la kigaidi la Daesh (ISIS) nchini humo na kusema, kuna mfungamano wa moja kwa moja baina ya magaidi wa Daesh na utawala pandikizi wa Israel.

Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni akiwajulia hali magaidi wanaofanya mauaji nchini Syria

 

Siku chache zilizopita, na licha ya wananchi wa Syria kuwa kwenye janga la miteteko mikubwa ya ardhi, magaidi makatili wa Daesh walifanya mashambulizi ya kikatili na kuua kwa akali watu 53 wakiwa mashambani.

Shirika rasmi la habari la Syria, SANA, liliripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, miili ya wahanga hao ilipelekwa katika hospitali ya serikali ya mji wa kihistoria wa Palmyra mkoani Homs.

Shirika hilo la habari lilieleza katika ripoti yake hiyo kuwa, raia hao walikuwa wanakusanya matunda mwitu katika jangwa la mkoa huo wakati walipovamiwa na magaidi wa ISIS na kufyatuliwa risasi ovyo.