Meli iliyobeba shehena ya silaha zilizotengenezwa Marekani yakamatwa katika Ghuba ya Uajemi
Feb 21, 2023 08:48 UTC
Kamanda wa walinzi wa mpakani wa jeshi la polisi la Iran ametangaza kuwa meli moja iliyobeba silaha za Marekani imekamatwa katika Ghuba ya Uajemi.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Tasnim, Brigedia Jenerali Ahmad Ali Goudarzi, kamanda wa walinzi wa mpakani wa jeshi la polisi la Iran amesema, meli moja imekamatwa katika mkoa wa Bushehr ikiwa na shehena ya visu vikubwa na mapanga zaidi ya 5,000.
Jenerali Goudarzi ameongeza kuwa, katika miezi michache iliyopita walinzi wa mpakani wa Iran wamegundua zaidi ya silaha 3,000 za kivita zilizokusudiwa kufikishwa mikononi mwa wafanyafujo na majambazi hapa nchini.
Kamanda wa kikosi cha ulinzi wa mpakani cha jeshi la polisi la Iran amesisitiza kuwa eneo la Ghuba ya Uajemi na Asia ya Magharibi si mahala pa kujifaragua jeshi la kigaidi la Marekani, na akasisitiza kwamba, vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vimekuwa na uwezo na nguvu kubwa zaidi kuliko ilivyokuwa huko nyuma na kwamba nguvu na uwezo huo unahisika waziwazi.
Kuanzia mwishoni mwa Septemba mwaka 2022, baadhi ya maeneo tofauti ya Iran yalishuhudia ghasia na machafuko; na tokea siku za kwanza kabisa, ilidhihirika jinsi baadhi ya vyombo vya habari vya jadi na vya kisasa vilivyohusika katika kueneza ghasia hizo.
Katika ghasia na machafuko hayo, viongozi wa kisiasa wa Marekani, wa utawala wa Kizayuni, wa baadhi ya nchi za Ulaya, vyombo vyao vya habari na vyombo vya habari vya Kifarsi vinavyoungwa mkono na nchi hizo za Magharibi waliwaunga mkono kwa kila hali wazusha machafuko na wavurugaji usalama wa taifa kwa kutumia kauli mbiu ya kuunga mkono haki za taifa la Iran.
Hatua za nchi za Magharibi na vyombo vya habari vyenye mfungamano na nchi hizo za kuzusha machafuko na kuvuruga usalama nchini Iran zilichukuliwa katika hali ambayo mamilioni ya wananchi wa Iran walijitokeza mara nyingi katika barabara na viwanja mbali mbali nchini kutangaza uungaji mkono wao kwa Mfumo tawala na nchi yao na kupinga vikali fujo na machafuko hayo.../