Iran yakosoa ukosefu wa misaada ya kimataifa kwa wakimbizi Waafghani nchini
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif ameikosoa jamii ya kimataifa kwa kutotoa misaada ya kutosha kwa ajili ya wakimbizi wa Afghanistan walioko nchini. Aidha amesisistiza kuhusu umuhimu wa kuandaa mazingira ya wakimbizi hao kurejeshwa kwa hiari nchini Afghanistan.
"Iran imewapa hifadhi wakimbizi Waafghani kwa zaidi ya miongo mitatu lakini la kusikitisha ni kuwa tumepokea misaada michache kwa ajili ya kuwahudumu," alisema Zarif Jumamosi mjini Tehran alipokutana na Kamishna Mkuu wa Wakimbizi Katika Umoja wa Mataifa Filippo Grandi.
Ameongeza kuwa kuna idadi kubwa ya wakimbizi halali na haramu kutoka Afghanistan wanaoishi nchini Iran na kuongeza kuwa: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa ikijaribu kuwapa wakimbizi huduma nzuri na imegharamika sana katika elimu ya wakimbizi."
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ametoa wito kwa Umoja wa Mataifa kutoa misaada ya kiuchumi kwa Afghanistan ili kupatikane nafasi za ajira zitakazowawezesha wakimbizi Waafghani kurejea makwao.
Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa Wakimbizi Katika Umoja wa Mataifa Filippo Grandi ameipongeza Iran kwa kuwa mwenyeji wa idadi kubwa ya wakimbizi. Amekiri kuwa Jamhuri ya Kiislamu imegharamika sana katika kuwahudumia wakimbizi kiafya na kielimu. Hivi sasa kuna takrabani watoto 350,000 Waafghani katika shule za umma nchini Iran.
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iran inakadiria kuwa kuna wakimbizi takribani milioni 3 kutoka Afghanistan wanaoishi katika maeneo mbali mbali ya Iran.