Shamkhani: Ushirikiano wa Ghuba ya Uajemi uchukue nafasi ya mifarakano na uhasama
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i95190-shamkhani_ushirikiano_wa_ghuba_ya_uajemi_uchukue_nafasi_ya_mifarakano_na_uhasama
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amesisitiza stratejia isiyobadilika ya sera za nje za Jamhuri ya Kiislamu kuhusu ushirikiano wa pande zote, endelevu na wenye manufaa na majirani zake na kusema: ili kuondokana na changamoto zilizopo ambazo kuendelea kwake hakuna maslahi kwa nchi yoyote katika eneo hili, ni lazima ushirikiano na mshikamano vichuke nafasi ya mifarakano na uhasama.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 16, 2023 22:57 UTC
  • Shamkhani: Ushirikiano wa Ghuba ya Uajemi uchukue nafasi ya mifarakano na uhasama

Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amesisitiza stratejia isiyobadilika ya sera za nje za Jamhuri ya Kiislamu kuhusu ushirikiano wa pande zote, endelevu na wenye manufaa na majirani zake na kusema: ili kuondokana na changamoto zilizopo ambazo kuendelea kwake hakuna maslahi kwa nchi yoyote katika eneo hili, ni lazima ushirikiano na mshikamano vichuke nafasi ya mifarakano na uhasama.

Ali Shamkhani mwakilishi wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na ambaye pia ni Katibu wa Baraza Kuu wa Usalama wa Taifa la Iran aliyeko safarini nchini Imarati amesema: Kuwepo hitilafu na hali ya kutoaminiana miongoni mwa nchi za eneo la kistatejia la Ghuba ya Uajemi ni kizuizi kikuu cha ustawi na uchumi wa eneo hilo na takwa la maadui wa nchi ajinabi. 

Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran ameeleza haya katika mazungumzo yake na Sheikh Tahnoun bin Zaid Al Nahyan Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati).

Ali Shamkhani na Shekh Tahnoun bin Zaid Al Nahyan 

Shamkhani ameongeza kusema kuwa, juhudi zinapaswa kufanyika ili kupanua na kuimarisha ushirikiano wa kisiasa, kiusalama, kiuchumi na kiutamaduni na kuzizuia nchi ajinabi kuchukua hatua zisizo na manufaa kwa kanda hii ya Ghuba ya Uajemi.   

Amesema, kubadilishana uwezo na tajiriba za kiuchumi, kibiashara na uwekezaji ni kati ya vipaumbele vikuu vya Jamhuri ya Kiislamu katika uhusiano wake na majirani zake na kwamba, kwa kuzingatia mazingira mazuri yaliyoandaliwa tangu mwaka mmoja uliopita kwa ajili ya kustawisha uhusiano kati ya Iran na Imarati, safari ya ujumbe wa Iran mjini Abu Dhabi ni mwanzo mwafaka kwa nchi hizo mbili kuingia katika awamu mpya ya uhusiano wa kisiasa, kiuchumi na kiusalama. 

Katika mazungumzo hayo, Sheikh Tahnoun bin Zaid Al Nahyan pia ameeleza kufurahishwa na ziara muhimu sana ya Admeri Ali Shamkhani katika Umoja wa Falme za Kiarabu na kusema kuwa, kushikiana na kuwa na urafiki na nchi kubwa na yenye nguvu ya Iran ni jambo muhimu na lenye thamani kubwa kwa Imarati.

Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Imarati amepongeza mapatano ya karibuni kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na utawala wa kifalme wa Saudi Arabia na kueleza kuwa, mapatano hayo yana jukumu kuu la kuimarisha amani, utulivu na usalama endelevu katika eneo la Magharibi mwa Asia.