Nasser Kanaani: Marekani haina ustahiki wa kuzungumzia haki za binadamu
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamuu ya Iran amesema kuwa, Marekani haina ustahiki wowote wa kuzungumzia haki za binadamu kutokana na historia yake chafu ya ukiukaji wa haki za binadamu.
Nasser Kanaani amesema kuwa, yaliyomo katika ripoti ya kila mwaka ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani kuhusiana na hali ya haki za binadamu nchini Iran hayana msingi wowote.
Amesisitiza kuwa, kile kilichokuja katika ripoti ya kila mwaka ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani kuhusiana na hali ya haki za binadamu nchini Iran hakina maana yoyote wala itibari na kwamba, Washington katu haina ustahiki na hhiajakidhi vigezo vya kuzunguumzia thamani aali za haki za binadamu katika mataifa mengine.
Kadhalika afisa huyo wa ngazi za juu katika Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameiponda ripoti hiyo na kuitaja kuwa ni upuuzi mtupu kwani imetawaliwa na utashi wa kisiasa huku ikiwa haina mashiko wala marejeo yoyote.

Nasser Kanaani ameashiria nafasi muhimu na ya juu ya haki za binadamu katika katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na katika kanuni zingine za kitaifa sambamba na jinsi Iran inavyoheshimu makubaliano na mikataba ya kimataifa.
Katika upande mwingine, Kanaani ameashiria ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu nchini Marekani na kuashiria muamala, unyama na vitendo vya mabavu vinavyofanya na vikosi vya usalama vya nchi hiyo dhidi ya raia bila kusahau ubaguzi wa wazi kabisa unaofanywa dhidi ya Wamarekani wenye asili ya Afrika.