Amir Abdollahian aishukuru Austria kwa kuwa mwenyeji wa mazungumzo ya kuondoa vikwazo
Hussein Amir- Abdollahian Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amezungumza kwa simu na Alexander Schallenberg Waziri wa Mambo ya Nje wa Austria na kupongeza kitendo cha Vienna cha kuwa mwenyeji wa mazungumzo ya kuondoa vikwazo.
Katika mazungumzo hayo ya simu ya wazi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amemshukuru mwenzake wa Austria kwa salamu na mkono wake wa kheri kwa mnasaba wa kuwadia mwaka mpya. Amir- Abdollahian aidha ameashiria umuhimu wa diplomasia na mazungumzo na kukaribisha ubunifu wowote wenye manufaa kutoka Austria kuelekea utambuzi sahihi wa matukio.
Kuhusu uhusiano kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Austria, Amir- Abdollahian ametaka kuendelezwa mashirikiano hayo kadiri inavyowezekana sambamba na kukumbusha nyanja mbalimbali za ushirikiano; ikiwemo kushirikiana katika sekta za tiba na dawa.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amegusia pia matukio ya Ukraine na akaeleza matarajio yae ya kuharakishwa mchakato wa kuhitimisha vita nchini humo na kuongeza kuwa: kjama alivyoeleza Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inapinga vikali kushiriki katika vita vya Ukraine.
Ameongeza kuwa, tumewaomba mara kadhaa viongozi wa Ukraine wawasilishe ushahidi na nyaraka kuhusu madai yao juu ya uwepo wa droni za Iran katika vita huko Ukraine.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Austria pia ametoa mkono wa kheri na kuwapongeza wananchi na serikali ya Iran kwa kuwadia Sikukuu ya mwaka mpya wa Kiirani wa Hijria Shamsia.
Alexander Schallenberg amekaribisha mapatano yaliyofikiwa kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Saud Arabia na kuyataja kama hatua moja mbele kwa ajili ya kupunguza mivutano katika eneo. Katika mazungumzo hayo ya simu, Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Austria wamejadili na kubadilishana mawazo pia kuhusu masuala ya kibalozikati ya pande mbili.