Watakaokiuka mapatano ya nyuklia ya Iran watajuta
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i9562-watakaokiuka_mapatano_ya_nyuklia_ya_iran_watajuta
Wabunge wa Iran leo wameonya kuwa watakaokiuka mapatano ya nyuklia yaliyofikiwa baina ya Iran na madola sita makubwa duniani watajuta.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jun 19, 2016 14:43 UTC
  • Watakaokiuka mapatano ya nyuklia ya Iran watajuta

Wabunge wa Iran leo wameonya kuwa watakaokiuka mapatano ya nyuklia yaliyofikiwa baina ya Iran na madola sita makubwa duniani watajuta.

Wabunge hao 237 wamebainisha msimamo wao katika barua walioandika kutangaza uungaji mkono wao kamili kwa kauli ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatollah Seyyed Ali Khamenei ambaye aliashiria vitisho vinavyotolewa na wagombea urais wa Marekani wanaojigamba kuwa watayachana makubaliano hayo iwapo wataingia madarakani - kama vitisho hivyo - vitatekelezwa kivitendo, basi wajue kuwa Jamhuri ya Kiislamu itayachoma moto kabisa makubaliano hayo ambapo kufanya hivyo nako ni katika kutekeleza amri ya Qur'ani Tukufu kuhusu majibu wanayopasa kupewa watu wanaokengeuka na kwenda kinyume na ahadi zao.

Katika barua yao, Wabunge wamesema, "iwapo upande wa pili utavunja ahadi zake, basi watakaofanya hivyo watapata somo ambalo hawatalisahau na tutalifanya dola la kiistikbari lijute kukiuka ahadi zake."

Agosti mwaka jana, mgombea mtarajiwa wa kiti cha urais kwa tiketi ya chama cha Republican nchini Marekani Donald Trum alijigamba kuwa, iwapo atachaguliwa kuwa rais, atauchana mkataba wa nyuklia baina ya Iran na madola sita makubwa duniani.

Makubaliano ya nyuklia ambayo yanafahamika kwa kifupi kama JCPOA na ambayo yalifikiwa Julai 14 mwaka uliopita kati ya Iran na nchi zinazounda kundi la 5+1 yamefungua ukurasa mpya katika uhusiano wa kisiasa na kiuchumi kati ya Tehran na nchi za Magharibi.