Iran na Russia zajadili mapatano ya kimkakati katika mazungmzo ya Moscow
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i95660-iran_na_russia_zajadili_mapatano_ya_kimkakati_katika_mazungmzo_ya_moscow
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian ameelezea matumaini yake kuwa makubaliano ya kimkakati ya ushirikiano na Russia yatakamilika ndani ya "chini ya mwezi mmoja."
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 29, 2023 07:53 UTC
  • Iran na Russia zajadili mapatano ya kimkakati katika mazungmzo ya Moscow

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian ameelezea matumaini yake kuwa makubaliano ya kimkakati ya ushirikiano na Russia yatakamilika ndani ya "chini ya mwezi mmoja."

Amir-Abdollahian ameyasema hayo leo Jumatano katika kikao na waziri mwenzake wa Russia, Sergei Lavrov, mjini Moscow na kuongeza kuwa, "Mazungumzo kuhusu mkataba wa ushirikiano wa kimkakati wa muda mrefu kati ya nchi hizi mbili yatakamilika nchini Russia na natumai katika muda wa chini ya mwezi mmoja."

Mnamo 2001, Tehran na Moscow zilitia saini mkataba wa ushirikiano wa miaka 10 ambao ulirefushwa hadi miaka 20.

Sasa, nchi hizi mbili zinataraji kutia sainia hati ya ushirikiano wa kimkakati ambayo itaainisha mustakabali wa mahusiano katika kipindi cha miaka ishirini ijayo.

Kadhalika katika matamshi yake, mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran amesisitiza kuwa uhusiano wa Iran na Russia unaendelea katika mkondo sahihi, akitumai kuwa ushirikiano wa pande mbili katika asasi za kieneo na kimataifa utaendelea kuimarika ipasavyo.

Lavrov kwa upande wake amesema mazungumzo kati ya Iran na Russia katika nyanja tofauti yanaendelea kikamilifu.

Amebainisha kuwa, uhusiano wa Tehran na Moscow katika nyanja za kisiasa, kibiashara, uwekezaji na kiuchumi pamoja na utekelezaji wa miradi muhimu unaendelea kuimarika.

Aidha amesema kumekuwa na ustawi wa kasi wa uhusiano wa pande mbili ndani ya mfumo wa tume ya pamoja ya kiuchumi huku akisema nchi mbili pia zimeonyesha ushirikiano wa karibu katika masuala ya kimataifa na kikanda.