12 Farvardin (Aprili 1); Siku ya Jamhuri ya Kiislamu
Leo Jumamosi tarehe 12 Farvardin, sawa na Aprili Mosi ni siku ya "Jamhuri ya Kiislamu", ambayo ni dhihirisho halisi la irada ya taifa kubwa la Iran katika kuthibitisha heshima na utukufu wa Uslamu pamoja na uamuzi wa wananchi wanamapinduzi wa Iran wa kujiainishia wenyewe hatima na mustakbali wa nchi yao.
Baada ya ushindi wa kishindo wa Mapinduzi ya Kiislamu chini ya uongozi wa Imam Khomeini (MA), mwezi Farvardin 1358 Hijria Shamsia (1979 Milaadia), kura ya maoni ya kukubali au kukataa kuanzishwa Jamhuri ya Kiislamu ilifanyika kote nchini Iran.
Kwa mujibu wa matokeo ya kura hiyo yaliyotangazwa tarehe 12 Farvardin 1358 Hijria Shamsia (Aprili 1, 1979), zaidi ya asilimia 98 ya watu walioshiriki katika kura hiyo ya maoni waliunga mkono kuanzishwa kwa Jamhuri ya Kiislamu.
Kwa mnasaba huo, Tarehe 12 Farvardin imetengwa katika kalenda ya Iran kuwa Siku ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Kwa kushiriki kwa wingi katika kura hiyo muhimu ya maoni ambayo kwa hakika ulikuwa ni uchaguzi wa kwanza katika historia ya mfumo mtakatifu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, wananchi shupavu wa taifa hili waliweza kuwathibitishia wazi na kivitendo walimwengu wote kuwa zama za uingiliaji wa kigeni na kufanyiwa maamuzi Wairani zilikuwa zimefikia tamati.
Vilevile, Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalitoa bishara njema ya uhuru na ukombozi kwa mataifa yanayodhulumiwa ili yafanye juhudi za kuweza kujinasua kutoka kwenye minyororo ya ukoloni na unyonyaji wa mfumo wa kibepari, na hivyo kutoa matumaini kwa watu walionyongeshwa na kudhulumiwa duniani. Yaliwapa moyo wa kujitawala na kupigania haki na uhuru maishani na kuwahakikishia kwamba hatimaye ni haki ndiyo itakayoshinda batili na uongo ulimwenguni.