Wairani washiriki mazishi makubwa ya maafisa wa IRGC waliouawa shahidi Syria
Makumi ya maelfu ya waombolezaji wamejitokeza mitaani jijini Tehran kutoa heshima zao kwa washauri wawili wa kijeshi wa Jeshi la Iran la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) ambao waliuawa shahidi katika hujuma ya kigaidi ya ndege za kivita za Israel karibu na mji mkuu wa Syria, Damascus.
Mazishi hayo yalianza asubuhi mjini Tehran ambapo waumini wamebebe majeneza ya mashahidi Milad Heidari na Meqdad Mehqani. Kamanda Mkuu wa IRGC Meja Jenerali Hossein Salami na Kamanda wa Kikosi cha Quds cha IRGC ni miongoni mwa maafisa wa ngazi za juu walioshiriki katika msafara wa mazishi.
Alfajiri ya kuamkia Ijumaa, ndege za kivita za utawala haramu wa Israel zilishambulia kwa makombora maeneo kadhaa ya mji mkuu wa Syria, Damascus. Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Syria, eneo la Al Dimas limeshambuliwa na ndege hizo za kivita za utawala vamizi wa Kizayuni.
Heidari, baba wa watoto wawili aliyekuwa na umri wa miaka 32, ni wa mkoa wa Kurdistan naye Mehqani, aliyekuwa na umri wa miaka 31, alifariki dunia kutokana na majeraha aliyoyapata wakati wa mashambulizi ya kigaidi ya Israel. Alikuwa kutoka Mkoa wa Golestan na alikuwa na mtoto wa miaka miwili.
Iran ilituma washauri wa kijeshi Syria kufuatia ombi rasmi la serikali ya nchi hiyo ili kuisaidia katika kukabiliana na makundi ya kigaidi yanayoungwa mkono na kufadhiliwa na madola ya kigeni. Mwaka 2017, msaada wa washauri wa kijeshi wa Iran uliisaidia Syria kuwashinda magaidi wakufurishaji wa Daesh ambao walikuwa wameteka maeneo mengi ya nchi hiyo.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran, Mohammad Mokhber amelaani vikali mauaji ya maafisa hao wa IRGC na kusema hujuma hiyo ya Israel nchini Syria ni kitendo cha ukiukaji wazi wa sheria za kimataifa.
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limesisitiza kuwa: bila ya shaka yoyote jinai za utawala bandia na mtenda jinai wa Israel hazitaachwa bila kujibiwa; na utawala huo haramu utalipa gharama za jinai zake.
Utawala wa Israel ni mmoja wa waungaji mkono wakuu wa makundi ya kigaidi ambayo yamekuwa yakipigana na serikali ya Rais Bashar al-Assad tangu kuzuka kwa wanamgambo na magaidi nchini Syria mapema mwaka 2011.