Mamilioni wakumbuka siku ya kufa shahidi Imam Ali (as)
Mamilioni ya Waislamu hususan wapenzi na wafuasi wa Watu wa Nyumba ya Mtume Muhammad (saw) kote duniani usiku wa kuamikia leo wameshiriki katika majlisi, vikao na mijumuiko ya kukumbuka tukio chungu la kufa shahidi Kiongozi wa Waumini, Imam Ali bin Abi Twalib (as).
Majlisi na vikao hivyo vya maombolezo ambavyo viliambatana na ibada za kuhuisha usiku wa Lailatul Qadr, vimekumbuka moja ya matukio machungu katika Uislamu ambapo Kiongozi wa Waumini na Imam wa mashariki na magharibii alikufa shahidi.
Majlisi za kukumbuka tukio chungu la kuuliwa shahidi Imam Ali bin Abi Twalib pia zinaendelea katika pembe mbalimbali katika ulimwengu wa Kiislamu.
Hapa nchini Iran mamilioni ya waumini wameshiriki katika shughuli hiyo katika miji mbalimbali na shughuli zote za umma zimefungwa leo kwa ajili ya kumuenzi na kumkumbuka Amirul Muuminin Ali bin Abi Talib (as).

Imam Ali bin Abi Twalib (as) alikufa shahidi tarehe 21 Ramadhani mwaka 40 Hijria siku mbili baada ya kupigwa upanga utosini na mtu aliyejulikana kwa jina la Ibn Muljim akiwa katika ibada ya Swala msikitini.
Ali bin Abi Twalib AS ambaye ndiye Imam wa kwanza katika mlolongo wa Maimamu 12 watoharifu, ni mume wa binti ya Mtume Fatma Zahra as na baba wa Maimamu wawili watoharifu Hassan na Hussein as.
Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatoa mkono wa pole kwa Waislamu wote ulimwenguni hususan wafuasi wakweli wa Ahlu-Baiti wa Mtume saw kwa mnasaba wa siku hii ya kukumbuka tukio chungu la kufa shahidi Imam Ali bin Abi Twalib as.