Iran yaipongeza Afrika kwa maadhimisho ya miaka 60 ya AU
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i97996-iran_yaipongeza_afrika_kwa_maadhimisho_ya_miaka_60_ya_au
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameyapongeza mataifa ya Afrika kwa mnasaba wa maadhimisho ya miaka 60 ya kuundwa Umoja wa Afrika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 26, 2023 06:47 UTC
  • Iran yaipongeza Afrika kwa maadhimisho ya miaka 60 ya AU

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameyapongeza mataifa ya Afrika kwa mnasaba wa maadhimisho ya miaka 60 ya kuundwa Umoja wa Afrika.

Katika ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter, Nasser Kan'ani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema: Miaka 60 baada ya ya kuundwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika, bara kubwa (la Afrika) linaadhimisha na kusherehekea mafanikio, umoja usio na kifani na uhuru."

Kan'ani ameeleza katika ujumbe wake huo kwamba, "Katika Siku ya Afrika, ninawanyooshea mkono wa salamu na pongezi marafiki na (wasemaji) wenzangu wa Kiafrika, nikiwatakia mustakabali wenye kung'aa, wenye ufanisi na amani."

Hapo jana Mei 25, bara la Afrika liliadhimisha miaka 60 tangu kuasisiwa kwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) na taasisi iliyoundwa baada yake, yaani Umoja wa Afrika (AU).

Si vibaya kuashiria hapa kuwa, siasa za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zimengeka katika misingi ya kuwa na uhusiano mzuri na nchi za dunia zikiwemo za bara la Afrika.

Viongozi wa Iran wamekuwa wakisisitiza kuwa, siasa kuu za Jamhuri ya Kiislamu ni kukabiliana na ubeberu wa kambi moja na kuhakikisha kila taifa linapewa haki ya kushiriki vilivyo katika masuala ya dunia na uhuru wa kujiamulia lenyewe mambo yake.