Jun 16, 2023 03:01 UTC
  • Raisi: Kuimarika ushirikiano wa Iran na Cuba kunawahamakisha mabeberu

Rais Ebrahim Raisi wa Iran amesema hatua ya kuendelea kuimarika na kupanuka ushirikiano wa Jamhuri ya Kiislamu na Cuba inayahamakisha madola ya kibeberu na ya kiistikbari duniani.

Rais wa Iran alisema hayo jana katika mazungumzo yake na mwenzake wa Cuba, Miguel Díaz-Canel mjini Havana na kuongeza kuwa, kuwa na uhusiano mzuri na wa karibu na nchi huru ni katika vipaumbele vya siasa za mambo ya nje za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Amesema kupigania uhuru na uadilifu na kupambana na madola ya kiistikbari ni sifa za pamoja za wananchi wa Iran na Cuba na kuongeza kuwa, Iran iko tayari kustawisha uhusiano wa pande mbili katika nyanja zote hususan katika uga wa sayansi na teknolojia.

Aidha Rais wa Iran jana jioni alikutana na kufanya mazungumzo na Rais wa zamani wa Cuba, Raul Castro ambapo wamelaani vikwazo haramu vya Marekani dhidi ya mataifa huru yanayopinga ubeberu kama vile Iran na Cuba.

Maafisa wa ngazi za juu wa Iran na Cuba jana Alkhamisi wakiwa mbele ya Rais Raisi na Rais Díaz-Canel, walisaini hati sita za kuimarisha ushirikiano wa nchi mbili katika nyuga tofauti kama vile tiba, teknolojia, mawasiliano na forodha.

Rais Raisi na Rais wa zamani wa Cuba, Raul Castro

Kadhalika nchi mbili hizi zimekubaliana kushirikiana zaidi katika uzalishaji wa chanjo mbalimbali hasa chanjo za kupambana na ugonjwa wa COVID-19.

Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, aliondoka mjini Tehran siku ya Jumatatu katika safari ya siku tatu ya kuzitembelea nchi za Amerika ya Kusini, zikiwemo Venezuela, Nicaragua na Cuba.

Sayyid Raisi ameondoka Havana, mji mkuu wa Cuba kurejea Iran, baada ya kukamilisha safari yake ya kuzitembelea nchi za eneo hilo la Amerika ya Latini.

Tags