"Maadui wa Waislamu hasa Israel, wamehamakishwa na ushirikiano wa Iran, Saudia"
(last modified Sun, 18 Jun 2023 04:40:55 GMT )
Jun 18, 2023 04:40 UTC

Rais wa Iran amesema kuimarika uhusiano na ushirikiano kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Saudi Arabia kumewahamakisha maadui wa Uislamu na Waislamu hususan utawala wa Kizayuni wa Israel.

Rais Ebrahim Raisi alisema hayo jana katika mazungumzo yake hapa mjini Tehran na Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudia Mwanamfalme Faisal bin Farhan na kuongeza kuwa, hatua ya kuhuishwa uhusiano wa Iran na Saudia ni pigo kubwa kwa Wazayuni ambao wameshindwa kuficha hamaki zao.

Rais wa Iran ameeleza bayana kuwa, nchi mbalimbali za kieneo na kimataifa hasa za Kiislamu zimeonesha hisia zao nzuri kuhusu makubaliano hayo ya kuanzishwa tena uhusiano wa kidiplomasia baina ya Iran na Saudia, lakini yamewaghadhabisha mno maadui.

Amesema Iran haina mipaka yoyote ya kuimarisha uhusiano na mataifa ya Kiislamu na kwamba, "Maadui tu Waislamu hasa utawala wa Kizayuni ndio waliohamakishwa na ushirikiano wa Iran na Saudia."

Itakumbukwa kuwa Iran na Saudi Arabia zilikubaliana mjini Beijing China Machi 10 mwaka huu kuhuisha uhusiano kati yazo na kufungua tena balozi za nchi mbili katika kipindi cha miezi miwili. 

Sayyid Ebrahim Raisi amesema utawala haramu wa Israel si tu ni maadui wa Wapalestina, lakini pia ni tishio kwa umma wote wa Kiislamu.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudia amesema Tehran na Riyadh zimeingia katika marhala mpya ya aina yake ya ushirikiano.

Aidha Faisal bin Farhan  ambaye aliwasili Tehran jana kwa ziara ya kwanza tangu mataifa haya mawili yenye nguvu ya Magharibi mwa Asia yakubaliane kurejesha uhusiano baina yao kufuatia kusitishwa kwa miaka saba, amemkabidhi Rais Raisi salamu kutoka kwa Mfalme Salman na Mohammed Bin Salman, Mrithi wa Ufalme wa Saudia.

Kadhalika Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Saudi Arabia amemkabidhi Sayyid Raisi mwaliko kutoka kwa Mfalme Salman, wa kumuomba aitembelee Saudia.

Tags