Jul 07, 2023 07:37 UTC
  • Ripoti yenye malengo maalumu ya Baraza la Haki za Kibinadamu dhidi ya Iran sambamba na ghasia za Ufaransa

Kamati eti ya kutafuta ukweli iliyoundwa na Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa kuhusu Iran imetoa ripoti yake ya awali kuhusu kile ilichokiita 'ukandamizaji wa Iran dhidi ya maandamano ya nchi nzima'.

Miezi 7 baada ya ghasia hizo, kamati hiyo iliyoundwa na Baraza la Haki za Kibinadamu imechapisha ripoti yake na kudai kwamba, Iran inapaswa kukomesha ukandamizaji wa watu wanaofanya maandamano ya amani na wimbi la kunyonga, kukamata watu na kuwaweka kizuizini baada ya kifo cha Mahsa Amini. Kamati hiyo pia imedai kuwa, haki za binadamu zitakuwa katika hatari ya kuporomoka zaidi iwapo kukamatwa na kunyongwa watu kutaendelea.

Ripoti hiyo imepingwa na kukosolewa na Iran na nchi nyingine huru katika mkutano wa Baraza la Haki za Kibinadamu la UN. Baada ya kusoma ripoti hiyo, nchi huru zilipinga kwa maneno kauli za upendeleo za wajumbe wa kamati hiyo na ripoti yao.

Jambo la muhimu ni kwamba msingi uliotegemewa katika kutayarisha ripoti hiyo sio sahihi, kwa sababu uhakiki wa maudhui ya ripoti hiyo unaonyesha kuwa, mstari mmoja baada ya mwingine umeandikwa kwa kutegemea taarifa za kughushi na potofu za vyombo vya habari vya lugha ya Kifarsi vya nchi za Magharibi na akaunti mahususi za mitandao ya kijamii zinazosimamiwa na kuendeshwa na idara za vita vya kisaikolojia za wapinzani wa Mapinduzi ya Kislamu. Vyombo vya habari na mawasiliano ya kijamii vya maadui wa Jamhuri ya Kiislamu na nchi za Magharibi vilikuwa na mchango mkubwa katika machafuko ya mwaka jana nchini Iran. 

Nukta muhimu ni kwamba, ripoti hii ni sehemu ya matunda ya vita mseto na vya pande zote ambavyo viliendeshwa dhidi ya taifa la Iran katika msimu wa mapukutiko (demani), na wahusika wake leo hii wanataka kuvuna matunda yake yote kupitia maonyesho na mchezo huo wa kuigiza katika ukumbi wa Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa.

Mwaka jana, wakati wa vita vikali vya pande zote, wapinzani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran walijaribu kugeuza maandamano ya kiraia ya baadhi ya wananchi na kuyafanya ghasia na machafuko kwa kuchochea maoni ya umma na kubadilisha fikra za raia kupitia mfululizo wa operesheni kubwa za kisaikolojia na vita vya utambuzi (cognitive warfare) kwa kutumia vibaraka wao wa ndani waliopewa mafunzo maalumu. Miezi 7 baada ya ghasia hizo na baada ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuvuka mgogoro huo, sasa maadui wanajaribu kutoa mashinikizo dhidi ya Iran kupitia taasisi za kimataifa. 

Nukta nyingine ya kuzingatiwa na kutiliwa maanani ni kwamba ripoti hiyo imetolewa sambamba na matukio mawili muhimu. Kwanza ni mabadiliko yaliyotokea katika siasa za kikanda za Iran na kupanuliwa uhusiano wa Tehran na nchi jirani. Pili ni ukatili wa kutisha wa polisi ya Ufaransa dhidi ya waandamanaji. Maonyesho hayo ya kuchekesha yamewekwa kwenye ukumbi wa Baraza la Haki za Binadamu la UN katika kipindi ambacho fikra za walimwengu zinashughulishwa na ukatili na ukandamizaji mkubwa wa serikali ya Ufaransa dhidi ya raia wa kawaida wanaopinga ubaguzi wa rangi na unyama wa polisi ya nchi hiyo baada ya mauaji ya kijana aliyekuwa na umri wa miaka 17 mwenye asili ya Afrika katika viunga vya Paris. Baya zaidi ni kwamba, hakuna tume wala kamati yoyote inayoundwa kuchunguza uhalifu na unyama wa polisi ya Ufarana na mabeberu wenzake, lakini pia wale wanaoandamana kupinga ukatili huo wanaitwa kuwa ni wanyama wa mwituni!  

Ghasia za Ufaransa

Naam, vyombo vya habari vya nchi za Magharibi kama CNN, BBC, France 24, DW na kadhalika ambavyo vilichochea, kupindua ukweli na viliyavalia njuga machafuko ya mwaka jana nchini Iran sasa vimeufyata mkia na kutia ulimi puani mbele ya ukatili na machafuko ya sasa huko Ufaransa. Hivi ndivyo vyombo vya habari vya nchi zinazodai kutetea haki za binadamu au kwa maneno sahihi saidi, zinazodai kuwa vinara wa haki za binadamu na demokrasia.  

Tags