Aug 02, 2023 10:40 UTC
  • Wazayuni wauvunjia heshima tena Msikiti wa al-Aqsa

Katika hatua ambayo imekuwa ni ya kawaida katika miezi ya hivi karibuni, Wazayuni kwa mara nyingine tena wameingia na kuuvunjia heshima Msikiti wa al-Aqsa kwa uungaji mkono wa jeshi la utawala ghasibu wa Isreal.

Msikiti wa al-Aqsa unajulikana kuwa nembo kuu ya utambulisho wa Kiislamu na Kipalestina wa eneo takatifu la Quds na utawala wa Israel unajaribu kuharibu utambulisho huo, lakini kusimama imara na kuwa macho wananchi wa Palestina kumeufedhehesha utawala huo wa Kizayuni na kupelekea njama zake kushindwa.

Ikiwa ni katika kuendeleza njama hizo leo Jumatano kundi moja la walowezi wa Kizayuni limeingia tena katika msikiti huo mtakatifu huku likiwa linapewa ulinzi na jeshi la utawala wa Kizayuni.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Isaac Wasserlauf, mmoja wa mawaziri wa baraza la mawaziri la Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala huo, pia alikuwa miongoni mwa Wazayuni  walioingia na kuuvunjia heshima msikiti huo mtakatifu.

askari wa Kizayuni wakivamia Msikiti wa al-Aqsa

Habari nyingine ni kuwa, wanajeshi wa Kizayuni leo wameshambulia eneo la al-Abassieh katika mji wa Sawan, kusini mwa Msikiti wa al-Aqsa.

Msemaji wa jeshi hilo ametangaza kutiwa mbaroni Wapalestina 9 katika maeneo tofauti ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kunyang'anywa silaha zao.

Wakati huo huo duru za ndani zimetangaza kuachiliwa huru vijana watatu kati ya wanne wa Kipalestina waliokamatwa asubuhi ya leo na wanajeshi wa Kizayuni katika shambulio la kambi ya wakimbizi ya Aqaba Jabr.

Ili kufikia malengo yao ya kujitanua katika ardhi za Wapalestina, Wazayuni kila siku hushambulia maeneo tofauti ya Palestina ambapo huua shahidi, kujeruhi au kuwakamata na kuwafunga jela Wapalestina wasio na hatia. Katika kujibu jinai hizo, Wapalestina nao hufanya operesheni za kulipiza kisasi dhidi ya Wazayuni.

Tags