Nov 30, 2023 03:52 UTC
  • Russia yailaumu Marekani kwa mgogoro wa Gaza

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia amesema Marekani inapasa kubebeshwa dhima ya mgogoro baina ya Palestina na utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Gaza.

Maria Zakharova, ameyasema hayo kwenye mahojiano aliyofanyiwa na idhaa ya Radio Sputnik na kuongeza kuwa, "Marekani ndiyo inayopasa kulaumiwa kwa hali ya sasa ya kuanguka mamlaka (ya Ukanda wa Gaza) na janga la mzozo baina ya Palestina na Israel."

Zakharova ameeleza bayana kuwa, siasa za kutowajibika za Washington ndizo zinafaa kulaumiwa kwa kushtadi mgogoro wa Ukanda wa Gaza. "Hakuna mwingine wa kubebeshwa dhima isipokuwa Marekani," amesisitiza Zakharova.

Mwanadiplomasia huyo wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia amebainisha kuwa, "Hakuna shaka sera za Washington ndiyo sababu kuu ya kuongezeka taharuki katika eneo (la Asia Magharibi)."

Kabla ya hapo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia ilisema kuwa, licha ya kuwepo onyo la kimataifa kuhusu kuongezeka idadi ya vifo vya raia katika Ukanda wa Gaza, siasa za Marekani katika eneo hilo umelilemaza Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Watoto ndio wahanga wakuu wa jinai za Israel Gaza

Kuongezeka uungaji mkono wa nchi za Magharibi na hasa Marekani kwa jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi wa Palestina kuliipa Israel uthubutu wa kushadidisha mashambulizi yake dhidi ya watu wasio na ulinzi wa Gaza.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imesema katika taarifa yake kwamba, wawakilishi wote wa Umoja wa Mataifa wanataka kusitishwa kikamilifu mapigano huko Gaza, lakini Marekani inatumia kura ya turufu katika Baraza la Usalama kukwamisha juhudi za kimataifa za kukomesha umwagaji damu Asia Magharibi.

Kuna wasiwasi kwamba, muda wa usitishaji vita uliongezwa kwa siku mbili nyingine ili kuwaachia huru wafungwa zaidi utakapomalizika, yumkini Wazayuni wakaanzisha tena mashambulizi yao ya kinyama dhidi ya Gaza mwishoni mwa wiki hii. 

    

Tags