Dec 02, 2023 06:05 UTC
  • Mauaji ya Wapalestina wa Gaza

Waziri wa vita wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel Yoav Gallant amesema, jana alisafiri kwa helikopta ya kivita katika Ukanda wa Gaza kuangalia mashambulizi ya jeshi la utawala huo, ambayo yalianza tena asubuhi baada ya Tel Aviv kutangaza kumalizika usitishaji mapigano wa wiki moja kwa sababu za kibinadamu.

Gallant ameandika katika akaunti yake ya X kwamba alisafiri kuelekea Gaza kwa helikopta ya kivita ili kushuhudia mashambulizi ya Israel katika eneo hilo na kwamba matokeo yalikuwa "ya kuvutia."
 
Waziri huyo wa vita wa utawala wa Kizayuni amesisitizia pia kile alichokiita umuhimu wa kuendelea kupambana na harakati ya Hamas, akidai kuwa harakati hiyo inaelewa lugha ya utumiaji nguvu tu.
 
Galant amerudia tena kutaja malengo unayofuatilia utawala wa Kizayuni katika mashambulizi yake ya kinyama unayoendeleza dhidi ya Gaza, ikiwa ni pamoja na kuiangamiza harakati ya Hamas, kusambaratisha uwezo wake wa kijeshi, na kuwakomboa mateka wa Israel wanaoshikiliwa na wanamuqawama wa Palestina katika eneo hilo.
Mashambulio mapya ya utawala wa Kizayuni Ukanda wa Gaza

Jeshi la utawala haramu wa Israel lilianzisha tena mashambulizi makali katika Ukanda wa Gaza mapema jana Ijumaa na kusababisha vifo vya mamia ya Wapalestina baada ya kutangaza kumalizika kwa usitishaji vita kwa ajili ya kufikisha misaada ya kibinadamu huko Gaza na kubadilishana mateka.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza, katika mashambulio hayo ya siku moja tu, Wapalestina wasiopungua 178 wakiwemo watoto wameuawa shahidi na wengine 589 wamejeruhiwa.

Utawala haramu wa Kizayuni wa Israel na Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS, zilikubaliana kwa upatanishi wa Qatar kusimamisha vita kwa muda wa siku nne, kulikoanza kutekelezwa Ijumaa iliyopita baada ya takribani siku 50 za vita. Usitishaji vita huo ulirefushwa mara mbili kwa siku mbili na hatimaye siku moja.../

 
 

 

Tags