Jan 13, 2024 11:50 UTC
  • Vituo vya kijeshi vya US vimeshambuliwa mara 130 na muqawama Iraq, Syria

Kambi na vituo vya muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Marekani katika nchi za Syria na Iraq vimeshambuliwa mara 130, tangu vilipoanza vita vya Gaza mnamo Oktoba mwaka uliopita.

Ripoti ya kanali ya televisheni ya al-Mayadeen ya Lebanon imewanukuu maafisa wa Marekani ambao hawakutaka kutaja majina yao wanaosema kuwa, ngome za kijeshi za Washington zimeshambuliwa mara 53 nchini Iraq, na mara 77 huko Syria katika kipindi hicho.

Wanajeshi 2,500 wa Marekani wapo nchini Iraq kwa kisingizio cha kutoa "mafunzo na ushauri". Aidha wanajeshi wengine wapatao 900 wa Washington wamewekwa katika maeneo tofauti nchini Syria kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi.

Haya yanajiri siku chache baada ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Iraq kutangaza kuwa, wanajihadi wake wamehusika na hujuma dhidi ya kambi hizo za wanajeshi vamizi wa Marekani katika nchi hiyo ya Kiarabu.

Hivi karibuni pia, gazeti la Washington Post la Marekani liliripoti kuwa, uungaji mkono wa US kwa Israel katika vita dhidi ya Gaza, pamoja na ongezeko la vifo vya raia wa Palestina, vimetoa motisha mpya kwa makundi ya ndani ya Iraq na Syria ya kufanya juhudi zaidi za kuyatimua majeshi ya muungano unaoongozwa na Marekani. 

Wanajeshi vamizi wa US wanavyoiba mafuta Syria

Lengo la operesheni za makundi ya muqawama dhidi ya ngome na vituo vya kijeshi vya Marekani limetangazwa kuwa ni kutoa mashinikizo kwa Ikulu ya White House ikomeshe uungaji mkono wake usio na kikomo kwa jinai za umwagaji damu zinazofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika vita dhidi ya Gaza

Zaidi ya Wapalestina 23,700 wameuawa shahidi tangu yalipoanza mashambulizi ya kinyama ya utawala wa Kizayuni Israel dhidi ya Wapalestina Gaza mnamo Oktoba 7 mwaka jana.

Tags