Jan 20, 2024 07:20 UTC
  • Jihadul Islami: Vikwazo vipya vya EU vimechochewa kisiasa

Harakati ya Jihadul Islami ya Palestina imeukosoa vikali Umoja wa Ulaya kwa kuwawekea vikwazo maafisa wa kundi hilo la muqawama pamoja na wenzao wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina(HAMAS).

Taarifa ya Jihadul Islami ya Palestina imesema, hatua hiyo ya EU imechochewa kisiasa, na inalenga kuunga mkono na kuukingia kifua utawala wa Kizayuni wa Israel unaoendelea kuuawa watoto wa Gaza.

Harakati hiyo ya muqawama yenye makao yake katika Ukanda wa Gaza imeeleza bayana kuwa, EU imetengaza vikwazo vipya dhidi yake na HAMAS kwa lengo la kujaribu kuficha na kudogosha mauaji ya kimbari yanayoendelea kufanywa na Wazayuni huko Gaza.

Taarifa ya Harakati ya Jihadul Islami ya Palestina imesisitiza kuwa, kundi hilo la muqawama litaendelea kuwalinda na kuwapa himaya Wapalestina, hadi ukombozi kamili wa taifa la Palestina.

Mapema jana Ijumaa, Baraza la Umoja wa Ulaya lilitangaza kuwawekea vikwazo maafisa kadhaa wa Jihadul Islami na HAMAS, kuzuia mali zao na kuwapiga marufuku kwenda katika nchi wanachama wa EU.

Kwa mujibu wa taarifa ya Baraza la EU, waliowekewa vikwazo hivyo vitakavyodumu hadi Januari 19 mwaka 2025 ni pamoja na Abdelbasit Hamza Elhassan Mohamed Khair, raia wa Sudan anayetuhumiwa kuufadhili mrengo wa muqawama wa palestina, Nabil Chouman na mwanawe wa kiume Khaled Chouman, wafadhili waandamizi wa HAMAS, Rida Ali Khamis, Musa Dudinna na raia wa Algeria Aiman Ahmad Al Duwaik.

Maandamano ya kuwaunga mkono Wapalestina

Hivi karibuni, Umoja wa Ulaya ulitangaza kumuweka Yahya Sinwar, kiongozi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) huko Gaza katika orodha yake ya magaidi, kwa tuhuma za kufanikisha shambulizi la kushtukiza la Kimbunga cha al-Aqsa la Oktoba 7 mwaka uliopita.

Ikumbukwe kuwa, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) tayari imewekwa katika orodha ya mashirika ya kigaidi ya EU.

Tags