Feb 19, 2024 11:06 UTC
  • Yemen: Tumeitwanga meli ya Uingereza na kuitungua ndege isiyo na rubani ya Marekani

Msemaji wa vikosi vya ulinzi vya Yemen ametangaza kuwa, katika kuonyesha mshikamano na uungaji mkono kwa taifa la Palestina na kujibu mashambulio na uchokozi wa Marekani na Uingereza dhidi ya ardhi ya Yemen, vikosi vya nchi hiyo vimeipiga makombora kadhaa meli ya Uingereza katika operesheni maalumu viliyotekeleza katika Ghuba ya Aden.

Kwa mujibu wa IRNA, Brigedia Jenerali Yahya Saree, msemaji wa jeshi la Yemen ametangaza habari hiyo leo na kuongeza kuwa makombora yaliyorushwa na Yemen yalilenga shabaha kwa umakini na kusababisha meli hiyo ya Uingereza kusimama.
 
Saree ameongeza kuwa, kutokana na ukubwa wa uharibifu, meli hiyo iko katika hatari ya kuzama katika Ghuba ya Aden.
 
Yahya Saree amesisitiza kuwa, operesheni za Yemen dhidi ya meli za utawala wa Kizayuni na zinazoelekea bandari za utawala huo haramu zitaendelea hadi pale vita dhidi ya Ukanda wa Ghazza vitakapokomeshwa na kuondolewa mzingiro lilioekewa eneo hilo.

Msemaji wa jeshi la Yemen ametangaza pia kwamba, vikosi vya nchi hiyo vimeitungua ndege isiyo na rubani ya Marekani aina ya MQ-9 katika mkoa wa Hudaidah magharibi mwa Yemen.

Shambulio la vikosi vya Yemen dhidi ya meli ya Uingereza limefanywa huku makao makuu ya kamandi ya vikosi vya kigaidi vya Marekani vilivyoko katika eneo la Asia Magharibi, Asia ya Kati na Afrika Mashariki yajulikanayo kama CENTCOM yakidai jana usiku kwamba maeneo yaliyo chini ya udhibiti wa Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen yameshambuliwa.

Tovuti ya Centcom imesema: makombora matatu ya cruise ya kutungua meli, nyambizi moja isiyo na rubani na ndege moja isiyo na rubani zimelengwa katika mashambulio hayo.

Marekani na Uingereza zimesha ishambulia Yemen mara kadhaa katika wiki za hivi karibuni.

Mashambulizi hayo yanafanywa kwa shabaha ya kuiwekea mashinikizo nchi hiyo ili isimamishe mzingiro wa majini iliouwekea utawala wa Kizayuni wa Israel.../

 

Tags