Feb 27, 2024 02:31 UTC
  • Kauli moja ya mirengo ya kisiasa ya Iraq kuhusu wajibu wa kuondoka wanajeshi wa kigeni nchini mwao

Qasim al-Araji, Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Iraq amesisitiza kuwa mirengo yote ya kisiasa ya nchi hiyo yanakubaliana kwa kauli moja kuhusu wajibu wa kuondoka wanajeshi wa kigeni nchini humo.

Licha ya kufanyika awamu kadha za mazungumzo ya kiistratijia baina ya Baghdad na Washington kwa ajili ya kuondoka kikamilifu wanajeshi wa Marekani nchini Iraq, lakini wanajeshi vamizi wa dola hilo la kiistikbari wanaendela kufanya ukaidi na wanatumia visingizio mbalimbali vya kuhakikisha hawatimuliwi nchini humo.

Baada ya kusambaratishwa genge la ukufurishaji la Daesh (ISIS) ambalo kimsingi liliundwa na kupewa silaha na mafunzo ya kijeshi na Wamarekani wenyewe, Bunge la Iraq lilipasisha muswada wa kulazimishwa kuondoka wanajeshi wote wa kigeni nchini humo. Katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni pia wananchi na vyama vya kisiasa vya Iraq vimekuwa vikihimiza mara kwa mara wajibu wa kufurushwa wanajeshi vamizi wa Marekani nchini mwao. Lakini wanajeshi magaidi wa Marekani wanaendelea kung'ang'ania kubakia nchini Iraq kwa madai ya kupambana na magaidi; kinyume kabisa na maafikiano yaliyofikiwa baina ya Baghdad na Washington.

Qasim al-Araji, Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Iraq

 

Matamshi ya hivi karibuni kabisa ya viongozi wa Iraq kuhusu wanajeshi wa kigeni walioko nchini humo ni yale ya Qasim al-Araji, Mshauri wa Usalama wa Taifa wa nchi hiyo ambaye alisema siku ya Jumamosi pambinzoni mwa Mkutano wa Sita wa Kimataifa wa Usalama Mjini Baghdad kwamba, wanajeshi na askari wa muungao wa kimataifa unaoongozwa na Marekani hawana sababu yoyote ya kuendelea kubakia nchini Iraq hivi sasa na hilo linahimizwa na kutiliwa mkazo na mirengo yote ya Iraq.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Iraq, Mohammed Shia' al-Sudani amesema kuwa, wanajeshi wa muungano wa kimataifa wakiongozwa na Marekani, lazima waondoke haraka kwenye ardhi ya Iraq kwani kuwepo kwao kunazidi kuhatarisha usalama wa nchi hiyo na eneo hili zima. Mwezi uliopita pia, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iraq ilisisitiza kuwa, kumefikiwa makubaliano ya kuanza kuondoka polepole wanajeshi na askari wa kigeni wanaoongozwa na Marekani na kwamba kila mwananchi wa Iraq wanataka wanajeshi hao wote waondoke haraka nchini humo.

Wanajeshi vamizi wa Marekani wanafanya jinai za kila namna ili wasitimuliwe nchini Iraq

 

Qasim al Tamimi, mchambuzi wa masuala ya kisiasa wa Iraq anasema: Vipigo angamizi wanavyopata wanajeshi wa Marekani kutoka kwa makundi ya muqawama wa Kiislamu ya Iraq yamewalazimisha wanajeshi hao vamizi kufanya mazungumzo kuhusu ratiba ya kuondoka nchini humo. Mchambuzi huyo ameendelea kusema, Marekani walirejea nchini Iraq mwaka 2011 kwa kisingizio cha kupambana na magaidi wa Daesh ambao ni wao wao Wamarekani ndio walioanzisha genge hilo na kulipa silaha na mafunzo ya kijeshi.  Amesema, wananchi wa Iraq wako macho na hivyo hawawezi kuruhusu Marekani kuendelea kubakia nchi humo akisisitiza kuwa, kila mtu ana yakini kwamba genge la kigaidi la Daesh ni tawi la Marekani la kujaribu kuhatarisha usalama wa Iraq na kupata kisingizio cha kuendelea kubakisha wanajeshi wake nchini humo.

Mwaka 2003, Marekani iliivamia kijeshi Iraq kwa madai ya kutafuta silaha za maangamizi ya umati ambazo haikuzipata hadi leo. Baada ya kuivamia nchi hiyo iliweka kambi yake huko Ain al Asad kwenye mkoa wa al Anbar wa magharibi mwa Iraq. Baada ya kupita miaka mingi ya kupindulia utawala wa Saddam na kutokomezwa genge la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS), hivi sasa hakuna kisingizio chochote kingine cha kuendelea kubakia wanajeshi wa Marekani na wa kigeni nchini humo. Lakini wanajeshi watenda jinai wa Marekani wanatafuta visingizio tofauti kujaribu kubakia nchini humo. Hata hivyo inavyoonekana ni kwamba hivi sasa viongozi na wananchi wa Iraq wamesimama imara kuhakikisha wanawafurusha wanajeshi hao kutoka nchini mwao. Hali ni hiyo hiyo iliyowakumba wanajeshi vamizi wa kigeni wakiongozwa na Marekani huko Afghanistan na si jambo lililo mbali kuona linajirudia nchini Iraq, kwa wanajeshi wote wa kigeni kutimuliwa nchini humo.

Tags