Ansarullah ya Yemen: Baada ya tuliyoizamisha, tutaendelea kuzishambulia meli za Uingereza katika Bahari Nyekundu
Yemen imeapa kuwa itaendelea kuzishambulia meli za Uingereza katika Bahari Nyekundu ili kuwaunga mkono Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza, ambao wamekuwa wakiandamwa na vita vya mauaji ya kimbari vinavyoendeshwa na utawala wa Kizayuni wa Israel kwa muda wa miezi mitano sasa.
Mamlaka za Yemeni zimeripoti kuwa meli ya Rubymar, ambayo ilikuwa imetelekezwa kwa siku 12, ilizama Ijumaa jioni wakati hali ya hewa ya dhoruba ilipotanda kwenye Bahari Nyekundu. Kamandi Kuu ya Majeshi ya Marekani (CENTCOM) ilitoa picha iliyoonyesha meli hiyo ikiwa imeelemea upande mmoja na kuthibitisha kuwa ilikuwa inazama.
Jeshi la Yemen limekuwa likizilenga meli za utawala wa Kizayuni Israel na zile zinazoelekea bandari za utawala huo haramu tangu mwezi Novemba mwaka jana kuonyesha mshikamano na Wapalestina wa Ghaza ambao kwa mwezi wa tano sasa wanaendelea kuandamwa na vita na mashambulio ya kinyama ya jeshi la Kizayuni ambayo hadi sasa yameshaua shahidi zaidi ya Wapalestina 30,320 wengi wao wakiwa wanawake na watoto na kujeruhi wengine 71,533.
Wayemen wametamka kinagaubaga kuwa hawatasita kufanya operesheni makini za kijeshi dhidi ya maslahi ya yeyote mwenye uadui na Yemen kwa ajili ya kulinda ardhi yao na kuthibitisha uungaji mkono wao usiotetereka kwa taifa la Palestina.../