Mar 27, 2024 07:39 UTC
  • Yemen yafanya mashambulizi 6 dhidi ya US, UK na Israel

Vikosi vya Jeshi la Yemen vimefanya mashambulizi sita dhidi ya meli za Marekani, Uingereza na utawala haramu wa Israel, ukiwa ni muendelezo wa operesheni za kuwaunga mkono wananchi madhulumu wa Palestina na kujibu uvamizi wa Washington na London dhidi ya Yemen.

Brigedia Jenerali Yahya Saree, Msemaji wa jeshi la taifa la Yemen alisema hayo jana Jumanne na kuongeza kuwa, katika kipindi cha siku tatu zilizopita, vikosi vya Yemen vimeshambulia manowari mbili za Marekani za 'APL Detroit' na 'Maersk Saratoga' katika maji ya Bahari Nyekundu.

Aidha vikosi vya Yemen vimeshambulia meli ya Uingereza ya 'Huang Pu' katika maji ya Bahari ya Shamu na nyingine ya 'Pretty Lady' ilipokuwa njiani ikielekea katika bandari za utawala wa Kizayuni unaokaliwa kwa mabavu ardhi za Palestina.

Brigedia Jenerali Saree ameongeza kuwa, Kikosi cha Anga cha jeshi la Yemen kimelenga pia na kusambaratisha meli mbili za kivita za Marekani katika Bahari Nyekundu. Amesisitiza kuwa, kuwa operesheni hizo dhidi ya 'pande tatu za uvamizi' zitaendelea maadamu hujuma na mzingiro dhidi ya Gaza unaendelea.   

Brigedia Jenerali Yahya Saree

Wakati huo huo, Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Iraq imeshambulia uwanja wa ndege na kambi ya kijeshi ya utawala wa Kizayuni wa Israel kwa kutumia ndege isiyo na rubani (droni).

Taarifa ya harakati hiyo imesema kuwa, katika operesheni ya kwanza, wanamapambano wake mapema leo Jumatano wameshambulia uwanja wa ndege wa jeshi la Israel wa Ovda kwa kutumia droni, na katika operesheni ya pili wamuqawama hao wameshambulia kituo cha kijeshi cha Speer katika ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Taarifa hiyo ya muqawama wa Kiislamu wa Iraq imeeleza kuwa, harakati hiyo itaendelea na mashambulizi yake dhidi ya maeneo ya utawala wa Kizayuni wa Israel hadi pale utawala huo utakapokomesha mauaji ya kimbari huko Gaza.

Tags