Apr 21, 2024 11:30 UTC
  • Kukandamizwa nchini Marekani wanafunzi wanaounga mkono Palestina

Polisi ya New York imewakamata zaidi ya wanafunzi 100 wanaounga mkono Palestina katika Chuo Kikuu cha Columbia ikiwa ni hatua ya wazi ya kuunga mkono jinai za utawala wa Kizayuni.

Jumatano asubuhi, mamia ya wanafunzi waliweka mahema katika Chuo Kikuu cha Columbia ikiwa ni hatua ya kupinga kuendelea jinai za kivita za utawala wa Kizayuni huko Ghaza na ushirikiano wa chuo hicho na makampuni yanayonufaika na ubaguzi wa rangi wa Kizayuni, hatua ambayo ilipelekea Polisi wa New York kuyaondoa mahema hayo kwenye chuo hicho Alkhamisi asubuhi  na kukamata idadi kubwa ya wanachuo hao, akiwemo binti wa mbunge mashuhuri wa Congress ya nchi hiyo. 

Hii ni katika hali ambayo, wanafunzi kadhaa walioshiriki maandamano hayo, akiwemo Esra Hirsi, bintiye Ilhan Omar, mwakilishi wa chama cha Democratic wa jimbo la Minnesota, walisema kwamba masomo yao yalisimamishwa kutokana na tuhuma mbalimbali zinazohusiana na uungaji mkono wao kwa Wapalestina.

Nemat Shafiq (kushoto), Mkuu wa cha Columbia akiwa katika kikao cha bunge

Siku chache zilizopita, Ilhan Omar alimuuliza rais wa Chuo Kikuu cha Columbia, Nemat Shafiq, katika kikao cha bunge kuhusu kukamatwa wanafunzi wanaounga mkono Wapalestina katika chuo kikuu hicho, ambapo Shafiq alitoa ushahidi kwamba harakati za wanafunzi hao zilikuwa dhidi ya Wazayuni.

Novemba mwaka jana, Chuo Kikuu cha Columbia kilisimamisha masomo ya makundi mawili ya wanafunzi ambayo yaliongoza maandamano ya kuunga mkono Palestina na kusitishwa vita huko Ukanda wa Gaza.

Tangu kuanza kwa mashambulizi ya kijeshi ya utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza, waungaji mkono wa wananchi wa Palestina wamekuwa wakifanya maandamano katika miji mikubwa ya Marekani, na vilevile katika vyuo vikuu hatua ambayo katika baadhi ya matukio, imesababisha kunyimwa nafasi za kazi baadhi ya wanafunzi waliounga mkono taarifa au Wapalestina wanaonyanyaswa na Wazayuni.

Maandamano ya wanafunzi wanaounga mkono Wapalestina Marekani

Hata hivyo mchakato wa kukandamiza maandamano ya wanafunzi dhidi ya Uzayuni nchini Marekani umeshika kasi huku harakati za wanafunzi pia zikikandamizwa kwa njia tofauti katika nchi za Ulaya. Katika tukio la hivi karibuni, mamlaka ya mji wa Lille nchini Ufaransa ilifuta kibali cha mkutano uliokuwa umepangwa kwa ajili ya kuwaunga mkono wananchi madhulumu wa Palestina.

Sambamba na kuongezeka uungaji mkono kwa haki za Wapalestina na vilevile maandamano ya kupinga jinai za mara kwa mara za utawala wa Kizayuni hususan katika Ukanda wa Ghaza, viongozi wa Marekani wameshadidisha ukandamizaji na kuwatia mbaroni wafuasi wa Palestina, wamepasisha sheria mpya zitakazobana na kuzuia zaidi mkusanyiko wowote wa kuunga mkono Palestina au kupinga jinai za Israel. Kuhusiana na suala hilo, Baraza la Wawakilishi la Marekani Jumanne lilipitisha sheria ya kulaani kauli ya "kutoka mtoni hadi baharini" iliyokuwa ikitolewa na waungaji mkono  wa haki za Wapalestina.

Katika sheria hiyo, iliyolaani kauli ya "Kutoka mtoni hadi baharini, na kuwa huru Palestina", ambayo imekuwa ikitumika sana nchini Marekani katika miezi ya hivi karibuni ya vita vya  Gaza, iliitaja hatua hiyo kuwa ni ya kibaguzi na iliyo dhidi ya Uzayuni. Azimio hilo lilipasishwa kwa kura 377 za kuunga mkono na kura 44 za kupinga. Sheria hiyo ni mojawapo ya sheria 17 za Warepublican walio wengi katika Baraza la Wawakilishi wanaunga mkono Israel, ambayo ilipigiwa kura katika siku za hivi karibuni.

Marekani, ikiwa muitifaki mkuu wa utawala wa Israel, hivi karibuni ilipinga kwa kura ya veto azimio la kupewa uanachama kamili Palestina katika Umoja wa Mataifa ikiwa ni katika sera zake za kukanyaga haki za Wapalestina kwa kutumia vibaya kura hiyo.

Ni dhahiri kwamba hivi sasa wanafunzi na kwa ujumla vijana wa Marekani wanapinga zaidi uungaji mkono wa pande zote wa nchi yao kwa utawala wa Israel na kuwataka wakuu wa nchi hiyo kutazama upya sera zao kuhusiana na jambo hilo. Uchunguzi uliofanywa pia unaonyesha kuwa vijana wa Wamarekani wakilinganishwa na wazee, wanaikosoa zaidi Israeli. Wanafunzi wa kizazi cha Z, ambao harakati yao imekuwa ni kama ile ya kupigania haki za watu weusi, mabadiliko ya hali ya hewa na kampeni za usalama wa bunduki, sasa wameungana na kuwa jumuiya kubwa inayodai uhuru wa Palestina, suala ambalo limekuwa changamoto muhimu kwa viongozi wa Washington kwa kadiri kwamba wanajaribu kuzuia kuenea kwake kwa kupitisha sheria mpya, kukandamiza na kuwakamata wanafunzi wanaoeneza kampeni hizo.