Apr 22, 2024 04:31 UTC

Harakati ya Mapamabano ya Kiislamu (Muqawama) ya Hizbullah ya Lebanon imesema wapiganaji wake wameiangusha ndege ya kisasa isiyo na rubani ya kivita na kijasusi ya utawala haramu wa Israel kusini mwa Lebanon baada ya kukiuka anga ya nchi hiyo.

Katika taarifa Jumapili, Hizbullah imesema imetungua ndege hiyo ya kivita ya Israel aina ya Hermes 450 katika eneo la al-Aishiya kusini mwa Lebanon.

Hizbullah imeongeza katika taarifa yake kwamba ndege hiyo isiyo na rubani ya Israel iliangushwa wakati "ilipokuwa ikiwashambulia wananchi waheshimiwa na wenye kusimama kidete."

Saa chache baadaye, jeshi la utawala haramu wa Israel lilikiri katika taarifa yake kwamba moja ya ndege zake zisizo na rubani ilitunguliwa kwa kombora la nchi kavu hadi angani wakati ikiwa katika operesheni kwenye anga ya Lebanon.

Ndege isiyo na rubani ya Hermes 450, ambayo imetengenezwa na kampuni ya Elbit ya Israel, hutumika kwa ajili ya ujasusi na inaweza pia kubeba hadi makombora manne.

Mpema mwezi Aprili pia wapiganaji shupavu wa Hizbullah walifanikiwa kutungua ndege ya kivita isiyo na rubani ya Hermes 900 ya Israel wakati ikiwa inakiuka anga ya Lebanon.

Ikiwa na mabawa ya mita 15, Hermes 900 ni ya pili kwa ukubwa ya kijasusi na kivita miongoni mwa ndege zisizo na rubani zinazomilikiwa na jeshi la anga la Israel.

Utawala haramu wa Israel umekuwa ukiendesha mashambulizi ya hapa na pale dhidi ya ardhi ya Lebanon tangu tarehe 7 Oktoba 2023 ulipoanzisha vita vya mauaji ya kimbari  dhidi ya Ukanda wa Gaza ambavyo hadi sasa vimeua Wapalestina karibu 34,100 wengi wao wakiwa wanawake na watoto.

Hizbullah imekuwa ikilipiza kisasi dhidi ya mashambulizi ya utawala huo, ikifanya operesheni za kila siku dhidi ya ngome za jeshi la Israel kwa mafanikio ili kuonyesha mshikamano na Wapalestina huko Gaza.