Nov 27, 2021 08:00 UTC
  • PLO yalaani makubaliano ya kijeshi ya Morocco na utawala wa Kizayuni wa Israel

Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) imelaani vikali makubaliano ya kijeshi yaliyofikiwa baina ya Morocco na utawala wa Kizayuni wa Israel na kueleza kuwa, mabaliano hayo ni zawadi kwa wavamizi.

Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) imesema katika taarifa yake kuwa, makubaliano ya kijeshi yaliyofikiwa baina ya Morocco na utawala vamizi wa Israel maana yake ni kukiuka maazimio ya mikutano na makubaliano baina ya mataifa mbalimbali ya Kiarabu na bila shaka yanakiuka dhahir shahir maslahi ya umma wa Kiarabu.

Sehemu nyingine ya taarifa ya Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) sambamba na kuashiria kwamba, wavamizi wanapaswa kuhitimisha ukaliaji wao wa kimabavu wa ardhi za Palestina na kutokubalika kwa utoaji zawadi wa aina yoyote ile kwa wavamizi na kuitaka Morocco ijitoe katika makubaliano yake na Israel.

Benny Gantz, Waziri wa Vita wa utawala haramu wa Israel (kulia) katika safari yake nchini Morocco

 

Makundi ya mapambano ya Kiislamu ikiwemo Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS na Jihadul-Islami yamelaani vikali makubaliano yaliyofikiwa kati ya Morocco na utawala haramu wa Kizayuni wa Isarel.

Makubaliano yamefikiwa na pande mbili katika safari ya Benny Gantz Waziri wa Vita wa Israel huko nchini Morocco. 

Wanaharakati mbalimbali katika mataifa ya Kiarabu na Kiislamu wameripotiwa wakilaani hatua ya Morocco ya kufikia makubaliano ya kiijeshi na utawala haramu wa Israel wakisema kuwa, hatua hiyo ni kuwasaliti wananchi madhulumu wa Palestina ambao wanakabiliwa na ukandamizaji kila uchao unaofanywa dhiidi yao na Wazayuni maghasibu.

Tags