Nov 17, 2022 02:20 UTC
  • Bunge la wazayuni washupalia vita zaidi katika historia ya Israel laanza kazi rasmi

Bunge jipya la utawala haramu wa Kizayuni wa Israel (Knesset) limeanza kazi rasmi huku vyombo vya habari vikilitaja kuwa ni Knesset ya "wenye misimamo mikali zaidi na washupalia vita zaidi" katika historia ya utawala huo.

Kwa mujibu wa gazeti la The Times of Israel, katika duru ya 25 ya uchaguzi wa Knesset, kwa mara ya kwanza bunge hilo limekuwa na wanawake wasiofika 36, ambapo idadi ya wanawake walioweza kuingia bungeni mara hii ni 29 tu.
Wabunge Waarabu katika Knesset ya sasa ni tisa tu, ambayo ni ndogo sana ikilinganishwa na idadi ya Waarabu zaidi ya milioni moja wanaoishi katika ardhi za Palestina inayokaliwa kwa mabavu (Israel).
Gazeti hilo la kizayuni limeendelea kuandika kuwa: kati ya wabunge 120 wa Bunge la Kizayuni, ni wajumbe 23 tu ambao ni wapya na waliosalia ni walewale wa zamani ambao wameweza kutetea viti vyao katika uchaguzi wa hivi majuzi.
Baadhi ya wabunge wazayuni washupalia vita na wenye misimamo ya kufurutu mpaka

Kulingana na ripoti hiyo, ni mbunge mmoja tu wa Knesset anayetoka jamii ya wachache ya Druze katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu na wabunge wengine watatu kati ya wote wanaowakilisha vyama 10 ndani ya Knesset ni 'mashoga'.

Gazeti la Kizayuni la The Times of Israel limeripoti kuwa, kauli mbiu za misimamo ya kufurutu mpaka na ilani kali za uchaguzi pamoja na kuwemo watu wenye mafungamano na Uzayuni wa kidini ni miongoni mwa sifa maalumu za bunge la sasa la utawala haramu wa Israel.
Tarehe 13 Novemba, rais wa utawala wa Kizayuni Yitzhak Herzog alimkabidhi rasmi Benjamin Netanyahu, kiongozi wa chama cha Likud jukumu la kuunda baraza la mawaziri baada ya kushinda uchaguzi wa Knesset.../

Tags