Umewahi Kusoma Hotuba ya Sha'baniyyah ya Mtume Muhammad (saw)?
(last modified Thu, 27 Feb 2025 13:22:54 GMT )
Feb 27, 2025 13:22 UTC
  • Umewahi Kusoma Hotuba ya Sha'baniyyah ya Mtume Muhammad (saw)?

Kwa mujibu wa kitabu cha “Kanzul-Maram fi A'mal Shahr al-Siyam”, Sheikh al-Saduq anamnukuu Imam Ridha (AS) akisema kwamba, katika moja ya siku za mwisho za mwezi wa Shaaban, kabla ya kuingia Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, Mtume Muhammad (SAW) alitoa hotuba inayojulikana kama al Khutbatu Al-Sha'baniyyah.

Katika hotuba hiyo Mtume SAW alibainisha fadhila za mwezi wa Ramadhani, miiko yake na namna ya kunufaika na fursa adhimu ya mwezi huo. Hotuba hiyo inasema:

Yaa Ayyuha-Naas (Enyi watu)! Kwa hakika umekujieni Mwezi wa Allah kwa baraka, rehma na msamaha; Mwezi ambao ni bora zaidi ya miezi mingine mbele ya Mwenyezi Mungu, na siku zake ni bora kuliko siku nyingine. Nyusiku zake ni bora kuliko nyinginezo, saa zake ndizo bora kabisa kuliko saa zote. Ni mwezi ambao ndani yake mmekaribishwa kuwa wageni wa Mwenyezi Mungu, na mmefanywa kuwa miongoni mwa watu waliokirimiwa na Allah. Pumzi zenu katika mwezi huu ni tasbihi, usingizi wenu humo ni ibada, amali zenu katika mwezi huo zinakubaliwa na dua zenu zinajibiwa. Basi, muombeni Mwenyezi Mungu, Mola wenu Mlezi, kwa nia ya kweli na nyoyo safi, akupeni taufiki ya kufunga mwezi huo na kukisoma Kitabu chake ndani yake. Kwa hakika, mtu muovu ni yule ambaye amenyimwa msamaha wa Mungu katika mwezi huu adhimu. Kumbukeni njaa na kiu ya Siku ya Kiyama kwa njaa na kiu ya mwezi wa Ramadhani, na toeni sadaka kwa mafukara na masikini miongoni mwenu. Waheshimuni wakubwa wenu, na muwahurumie wadogo miongoni mwenu. Ungeni udugu, na mzilinde ndimi zenu. Fumbeni macho yenu mbele ya yote yasiyoruhusiwa kutazamwa, na msisikilize yasiyoruhusiwa kusikilizwa. Wahurumieni mayatima wa watu, ili mayatima wenu pia waonewe huruma. Muombeni Allah msamaha wa madhambi yenu, na nyoosheni mikono yenu kwake kwa dua katika nyakati za Swala, kwani hizo ndizo saa bora zaidi ambamo Allah SW huwatazama waja wake kwa jicho la rehma; Huwajibu wanapomuomba na huitikia wanapomuita, na hutakabali maombi yao wanapomtaradhia.

Enyi watu! Kwa hakika nafsi zenu zimewekwa rehani kwa amali zenu, zikomboeni kwa istighfari. Migongo yenu imelemewa kwa uzito wa madhambi yenu, punguzeni uzito huo kwa kurefusha sijda zenu, na mjue kuwa Allah SW ameapa kwa Ukuu Wake kwamba hatawaadhibu wanaoswali na wanaosujudu, na kwamba hatawatisha kwa moto siku ambayo watu watasimama mbele ya Mola Mlezi wa walimwengu wote..

Enyi watu! Atakayemfuturisha aliyefunga Saumu katika mwezi huu atapata thawabu za kumwachia uhuru mtumwa, na kusamehewa madhambi yaliyopita.

Masahaba walisema: “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Sisi sote hatuna uwezo wa kufanya hayo.” Mtume (saw) alisema: "Jiepusheni na moto wa Jahannam walau kwa kulisha mtu kipande cha tende, jiepusheni na moto hata kwa kumpa mtu maji. Mwenyezi Mungu atatoa thawabu hizo kwa yeyote anayefanya kazi hizi ndogo, kwani hana uwezo wa zaidi ya hayo."

Enyi watu! Atakayeboresha tabia zake katika mwezi huu, atarahisishiwa kupita juu ya Siraat, siku ambayo miguu ya watu itatetemeka. Na mwenye kupunguza mzigo wa waliochini yake katika mwezi huu, Mwenyezi Mungu atamfanyia wepesi hisabu yake Siku ya Kiyama. Na mwenye kuzuia shari yake kwa watu, basi Allah atamwepusha na ghadhabu Zake siku atakapokutana Naye. Yeyote atakayemkirimu yatima katika mwezi huu, Allah atamkirimu Siku ya Kiyama, na atakayewatendea wema ndugu na jamaa zake, basi Allah atamjaalia rehma Zake Siku ya Kiyama. Na yeyote atakayevunja udugu na ndugu zake, Allah pia atamkatia rehma zake Siku ya Kiyama. Atakayeswali Swala za Suna katika mwezi huu, Allah SW atamwepusha na moto wa Jahannam. Na yeyote Atakayefanya jambo la faradhi ndani ya mwezi huu atapata ujira wa mwenye kutekeleza faradhi sabini katika miezi mingine. Atakayezidisha kuniswalia mimi ndani ya mwezi huo, Mwenyezi Mungu ataifanya mizani yake kuwa nzito siku ambayo mizani itakuwa nyepesi. Na yeyote atakayesoma Aya moja ya Qur’ani katika mwezi huu, atapata thawabu za mtu aliyehitimisha Qur’ani nzima katika miezi mingine.

Enyi watu! Hakika milango ya Pepo ipo wazi katika mwezi huu, hivyo muombeni Allah asiwafungie milango hiyo. Vilevile, milango ya moto wa (Jahannam) imefungwa katika mwezi huu, hivyo muombeni Allah SW asiwafungulie milango hiyo. Mashetani wamefungwa kwa minyororo katika mwezi huu, muombeni Mola wenu hao mashetani wasije kuwa na satuwa juu yenu.

Amirul-Muuminina Ali bin Abi Twalib (as) alisema: Nilisimama na kusema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Ni amali gani bora katika mwezi huu? Akasema: Ewe Abul-Hassan! Amali bora zaidi katika mwezi huu ni kujiepusha na makatazo ya Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Kisha Mtume (saw) akalia, nikasema: Yaa Rasulallah! Ni nini kinachokuliza? Akasema: Ewe Ali! Nalia kwa sababu ya yale utakayofanyiwa katika mwezi huu. Kana kwamba nakuona ukiswali kwa ajili ya Mola wako Mlezi, kisha atakujia muovu zaidi wa watu wa wote wa zote, za awali na za mwisho, ndugu wa aliyekata miguu ya ngamia jike wa Thamud, na kukupiga panga kwenye utosi wako, hadi ndevu zako zilowane kwa damu.

Amirul-Mu’minin Ali (as) akasema: Nilisema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Wakati huo dini yangu itakuwa salama? Akasema (saw): “Dini yako itakuwa salama.” Kisha akasema: Ewe Ali, anayekuua wewe ameniua mimi, anayekuchukia amenichukia mimi, na anayekutukana wewe amenitukana mimi. Kwa sababu wewe kwangu mimi ni kama nafsi yangu, roho yako inatokana na roho yangu na udongo wako umetokana na udongo wangu. Mwenyezi Mungu aliyetukuka, aliniumba mimi na wewe, akaniteua mimi na wewe, na akanikhitari mimi kuwa Mtume, akakuchagua wewe kuwa Imam. Anayekana Uimamu wako huwa amekana Utume wangu. Ewe Ali! Wewe ni wasii wangu, baba wa wanangu, mume wa binti yangu, na Khalifa wangu juu ya umma wangu, wakati wa uhai wangu na baada ya kufariki dunia kwangu. Amri yako ni amri yangu, na katazo lako ni katazo langu. Naapa kwa jina la aliyenipa Utume na akanijaalia kuwa mbora wa viumbe kwamba wewe ni huja wa Mwenyezi Mungu juu ya viumbe vyake, na mwaminifu wa siri yake, na Khalifa wake kwa waja wake.

Kisha Mtume aliimuuliza Amirul Muuminina: Utastahimili vipi kuuawa? Akasema (as) kwamba: “Kuuawa hali dini yangu iko salama si jambo la kumfanya mtu kuwa na ustahamilivu, bali ni jambo la kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa ajili yake.”