Ramadhani; Mwezi wa Dhifa ya Mwenyezi Mungu (1)
(last modified Mon, 10 Mar 2025 07:10:12 GMT )
Mar 10, 2025 07:10 UTC
  • Ramadhani; Mwezi wa Dhifa ya Mwenyezi Mungu (1)

Assalaam alaykum wapenzi wasikilizaji. Tumo katika siku tukufu za ibada ya funga ya mwezi wa Ramadhani na sote tumealikwa kuwa wageni wa Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Mtu anapoalikwa kwenye karamu au shughuli yoyote ya ugeni, hali hiyo humsisimua na kumfanya awe ni mwenye furaha wakati wote hadi wakati wa kushiriki karamu au ugeni huo. Kwa mnasaba wa kuwadia mwezi mtukufu wa Ramadhani tumeakuandalieni vipindi maalumu ambapo kipindi hiki kitakuwa kikujieni kila siku kikiwa na anuani ya Ramadhani; mwezi wa dhifa ya Mwenyezi Mungu. Sambamba na kumuomba Mwenyezi Mungu azitakabali funga na ibada zenu katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani tuna matumaini kwamba, mtanufaikka na vipindi hivi hii ikiwa ni sehemu ya kwanza ya mfululizo huu.

 

******

Wapenzi wasikilizaji tunakianza kipindi chetu hiki kwa Aya ya 185 ya Surat al-Baqarah inayosema:

 شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِی أُنزِلَ فِیهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِّلنَّاسِ وَبَیِّنَاتٍ مِّنَ الْهُدَىٰ وَالْفُرْقَانِ

Ni Mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa humo Qur´ani kuwa ni uwongofu kwa watu, na hoja zilizo wazi za uwongofu na upambanuzi.

Sote tunajua ya kwamba jambo linalomfanya mwalikwa kuwa na furaha ya ugeni ni ile hamu ya kutaka kukutana na mwenyeji wake pamoja na wageni wengine walioalikwa kwenye karamu hiyo ambapo mazingira mapya ya kuonana na kujuliana hali wageni hujitokeza, mapenzi na upendo kudhihirishwa na wakati mwingine zawadi kutolewa na mwenyeji wao. Kabla ya kushiriki kwenye mwaliko, jambo la kwanza ambalo mwalikwa hukabiliana nalo ni jinsi atakavyovaa vizuri, kutembea vizuri na kuzungumza vizuri. Tunapofahamu kuwa mwenyeji wetu atakuwa anatusubiri mlangoni kwa ajili ya kutulaki, hapo kasi ya hatua hatua zetu kumuelekea huongezeka. Mwanzo wa kila mwaliko huwa ni kuzingatia na kufungamana kimawazo na mwenyeji, ambapo kila mara mfungamano huo unapokuwa ni wa kirafiki zaidi, ugeni nao hunoga na kuvutia zaidi. 

Sasa ikiwa mialiko na ugeni wa kawaida wa baina yetu huwa na shauku namna hii vipi mja anapoambiwa kuwa, umealikwa kuwa mgeni wa Mwenyezi Mungu? Hivi sasa na kwa mara nyingine tumealikwa na mwenyeji ambaye ni rafiki mwema wa kuvutia, mwenye huruma na anayesamehe zaidi kati ya wenyeji wengine wote tunaowajua sisi wanadamu. Mwenyezi Mungu ni Muumba wa pekee na Mwenye Hekima ambaye jina lake hutuliza nyoyo zinazosononeka na kutaabika.

Kwa mara nyingine tena milango ya mbinguni imefunguliwa wazi mbele ya waumini ili wapate kuzijua nafsi zao na Muumba wao katika mazingira tulivu na yaliyo mbali na mahangaiko na pilikapilika za kila siku maishani. Katika zama hizi za maisha ya kisasa ambapo mwanadamu amepokonywa kabisa fursa ya kufikiria juu ya nafsi yake na hivyo kumfanya kuwa kiumbe anayezingatia tu masuala ya kimaada, Ramadhani ni fursa nzuri ambayo humuandalia mwanadamu huyu mazingira mazuri ya kufikiria juu ya nafsi yake mbali na shughuli zake nyingi za kila siku maishani. Kwa ibara nyingine ni kuwa mwezi huu mtukufu humuandalia mwanadamu fursa ya kufikiria juu ya shughuli za ndani ya nafsi yake kinyume na miezi mingine ya mwaka ambapo huwa anajishughulisha zaidi na masuala ya nje ya nafsi yake. Hali hiyo humuwezesha kuwaza na kufikiria sehemu za ndani ya nafsi yake ambazo anapasa kuzirekebisha na kuziboresha, kuwaza juu ya Muumba wake na kumuomba Yeye tu msaada bila ya kuwategemea viumbe wengine. Mwezi wa Ramadhani kwa mujibu wa Qur'ani Tukufu na maneno ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) pamoja na Maimamu watoharifu wa Nyumba yake (as), ni mwezi ambao ni bora kuliko miezi mingine yote ya mwaka. Inatutosha kutazama moja kati ya majina ya mwezi huu mtukufu ili tupate kujua heshima na utukufu wake mkubwa. Mwezi huu umetajwa kuwa ni 'Shahrullah' kwa maana ya Mwezi wa Mwenyezi Mungu.

******

Sote tunafahamu vyema kwamba miezi yote ni ya Mwenyezi Mungu lakini ni mwezi mmoja tu kati ya miezi hiyo ndio umetajwa kuwa ni Mwezi wa Mwenyezi Mungu. Vilevile tunajua kwamba nyusiku zote ni za Mwenyezi Mungu lakini ni usiku mmoja tu kati ya nyusiku hizo ndio umetajwa kuwa na utukufu mkubwa zaidi kwa kupewa jina la Lailatul Qadr, usiku wa cheo kitukufu ambao unapatikana kwenye mwezi huu mtukufu wa Ramadhani. Ramadhani ni mwezi wa ugeni ambao mwenyeji wake ni Mwenyezi Mungu mwenyewe, na ambaye amewaalika watu wote kushiriki. Ugeni huu sio kama Hija ambapo waalikwa ni wale tu walio na uwezo wa kushiriki, wala Khumsi na Zaka ambayo hutozwa faida ya ziada kwa mazao, na wala hata Swala ambayo imewajibishwa kwa Waislamu katika siku zote na katika kila hali.

Moja ya mambo ambayo yana adhama kubwa na kutofautisha mwezi mtukufu wa Ramadhani na miezi mingine ya mwaka ni jinsi Mwenyezi Muungu anavyotoa malipo ya amali njema katika mwezi huu adhimu na mtukufu. Katika sehemu moja ya hotuba yake ya Shaaban ya kuukaribisha mwezi mtukufu wa Ramadhan, Mtume (saw) alinukuliwa akisema:

 Enyi watu! Hakika mwezi wa Mwenyezi Mungu umekufikieni kwa baraka, rehema na msamaha. Mwezi ambao mbele ya Mwenyezi Mungu, ni mwezi ulio bora zaidi, siku zake ni siku bora zaidi, nyusiku zake ni nyusiku bora zaidi na saa zake ni saa bora zaidi. Ni mwezi ambao ndani yake mmealikwa kuwa wageni wa Mwenyezi Mungu (katika dhifa yake) na kufanywa kuwa miongoni mwa watu wanaonufaika na ukarimu Wake. Pumzi zenu katika mwezi huu ni tasbihi, usingizi wenu ni ibada, amali zenu zinakubaliwa na dua zenu kujibiwa.

Waislamu wamehimizwa kusoma kwa wingi kitabu kitukufu cha Qur'ani. Kusoma Aya moja ya Qur'ani ndani ya mwezi huu mtukufu malipo na thawabu zake ni mara kadhaa ikilinganishwa na miezi mingine.

Pamoja na hayo yote, swali ambalo daima limekuwa likiulizwa ni kwamba, kwa nini Mwenyezi Mungu aliuchagua mwezi huu na kuufanya kuwa mwezi wa kushuka Qur'ani ndani yake?

Jambo la kuvutia ambalo wapenzi wasikilizaji mnapaswa kulifahamu ni kuwa, vitabu vingine vya mbinguni pia vilishushwa ndani ya mwezi wa Ramadhani. Imam Ja'afar Swadiq (as) amenukuliwa akisema: Torati ilishushwa tarehe 6 Ramadhani, Injili iliteremeshwa tarehe 12 Ramadhani, Zaburi ilishushwa 18 Ramadhani na Qur'ani ilishushwa katika Laylatul-Qadr.

Kwa upande mwingine, mwezi wa Ramadhani ni mwezi wa malezi ya mwanadamu, na malezi hayawezekani bila elimu. Ni kwa sababu hii, inafaa kuandaliwa mipango ya kimalezi ya Saumu na uchaji Mungu na hilo likawa linaafikiana na mafundisho ya mbinguni ya Qur'an Tukufu. Kitabu kile kile ambacho ni kitabu cha mwongozo na nuru. Kitabu ambacho kinatoa onyo na indhari na wakati huo huo kinatoa bishara na khabari njema.

Mwenyezi Mungu anasema katika Aya ya 51 ya Surat An'am:

Na waonye kwayo wanao ogopa kuwa watakusanywa kwa Mola wao Mlezi, hali kuwa hawana mlinzi wala mwombezi isipo kuwa Yeye, ili wapate kuwa na takua.

*******

Mwezi mtukufu wa Ramadhani mbali na waja kualikwa katika ugeni wa Mwenyezi Mungu, masiku haya matukufu ni fursa adhimu ya kujitakasa nafsi. Ni mwezi ambao ndani yake mja anaweza kunufaika pakubwa na nyusiku zake kwa kufanya ibada na hivyo kuchuma na kujiandalia masurufu kwa ajili ya safari ya kuelekea kwa Mola. Mwezi huu ni fursa ya dhahabu ya mja kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu kwa kufabnya ibada, kusoma, Qur'ani dua na kunong'ona na Mola Muumba hususan nyakati za usiku.

Tunakamilisha kipindi chetuu cha leo kwa kutupia jicho kwa muktasari dua ya sikuu ya kwanza ya mwezi wa Ramadhani ambayo inasema:

Ee Mwenyezi Mungu! Kujaalie kufunga kwangu katika mwezi huu kuwe ni kufunga kwa wanaofunga (Saumu zao zikawa sahihi na kukubaliwa). Na kusimama kwangu kwa ajili ya ibada kuwe sawa na wanaofanya ibada (zao zikapokelewa), na Uniepushe na usingizi wa wavivu, niwezeshe niukamilishe Ewe Mola wa Walimwengu, na Uniafu Ewe Mwenye kuwasamehe wakosaji.

Katika dua hii tunamuomba Allah aifanye Saumu na funga yetu iwe ni funga ya wanaofunga kwa njia sahihi. Kwa maana kwamba, iwe ni funga barabara ambayo si ya kuacha ula na kunywa tu kama wanavyodhani wengi wetu, bali anapofunga mtu awe amefunga macho, masikio, na mwili wake mzima. Asisikie visivyopaswa kusikiliza na asitazame vilivyoharamishwa kutazamwa. Asisengenye au kusema uongo, asimzulie na kumzushia mtu na kadhalika. Kwa kufanya hivi atakuwa amefunga funga ya wanaofunga kwa njia sahihi.

Katika sehemu nyingine ya dua ya kwanza ya mwezi wa Ramadhani tunamuomba Allah atujaalie kusimama kwetu kwa ajili ya ibada kuwe sawa na wanaofanya ibada (zao zikapokelewa), na atuepushe na usingizi wa wavivu, na atuwezeshe tuikamilishe. Katika sehemu hii ya dua pia kuna nukta kadhaa muhimu za kuashiria lakini kutokana na kumalizika muda wa kipindi hiki, sina budi kukomea hapa nikukutakieni Ramadhan Karim na Swaum Maqbul....

Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.