Ramadhani, Mwezi wa Dhifa ya Mwenyezi Mungu (6)
Mwezi mtukufu wa Ramadhani ni kama ilivyo mvua ya msimu wa machipuo, inayonyesha kwenye jangwa kavu lenye kiu ya maji. Jongeeni tukidhi kiu ya nyoyo zetu kwa maji ya mvua hii ya uzima.
Kuna fursa nyingi na za kipekee katika mwezi huu mtukufu ambazo zinaweza kutuandalia mazingira safi ya kuepuka na kutatua changamoto nyingi zinazotukabili maishani. Hata kama nyakati za mwanga za mwezi wa ramadhani hupita kwa kasi lakini nyakati hizi takatifu hutukumbusha miadi yetu na Mwernyezi Mungu na kutuainishia njia nyoofu ya maisha. Kama ambavyo tumekuwa tukisisitiza katika vipindi hivi maalumu, mwezi wa Ramadhani ni mwezi wa machipuo ya ibada, mwezi ambao milango ya Mwenyezi Mungu imefunguliwa mbele ya waja wake na ni mwezi ambao hutupa fursa za kipekee za kuweza kujirudi na kutambua hakika ya dhati zetu. Njooni tuandamane pamoja katika safari hii ya kimaanawi na kiroho ili tupate kunufaika na baraka na fadhila za mwezi huu mtukufu kupitia dua na ibada zake zenye malipo makubwa mbele ya Mwenyezi Mungu.
***********
Tumeingi katika siku ya 17 ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Katika siku kama hizi, Mwenyezi Mungu alimuongoza mja wake, Muhammad Mustafa (saw), kutoka Masjid al-Haram hadi Masjid al-Aqswa na kutoka hapo hadi kwenye mbingu ya saba ili kumuonyesha dalili na siri za ghaibu na hivyo kumpa hadhi na heshima zaidi. Safari hii ya kiroho huitwa mi'raaj au kupaa mbinguni.
Mi'raaj ni safari ya mbinguni ya Mtume Mtukufu (saw). Safari ambayo hakika yake anaijua mja huyo pekee mkamilifu wa Mwenyezi Mungu. Safari hiyo ya mbinguni ilianzia ardhini na kisha Mtume (saw) akawa amesafiri hadi mbingu ya saba, kisa ambacho kimezungumziwa kwa ufupi na kwa namna ya mafumbo katika Sura ya Najm ya Qur'ani Tukufu. Katika safai hiyo ya mbinguni , Mtume (saw) alisafiri na kufika sehemu ambayo hata Malaika Jibril mwenyewe hakuruhusiwa kufika na kuweza kuzungumza na Mwenyezi Mungu Muumba wa mbingui na ardhi. Sehemu ya safari hiyo takatifu imesimuliwa na Mtume mwenyewe katika Kisa cha Mi'raaj. Sehemu ya kisa hicho inasema kwamba Mwenyezi Mungu alimuhutubu Mtume (saw) kwa kumwambia: "Ewe Ahmad! Je, unajua mja huwa amenikaribia katika hali gani? Mtume akamjibu: Ewe Mwenyezi Mungu! Sijui. Mwenyezi Mungu akasema: Anapokuwa katika hali ya njaa au kusujudu." Kwa maneno haya tunatambua kwamba funga ya mwezi wa Ramadhanii hata kama huambatana na njaa na kiu lakini njaa hiyo humkurubisha mwanadamu kwa Mwenyezi Mungu. Hivyo ni jambo zuri lililoje tuiambatanishe njaa na kusujudu huku na ibada nyingine za mwezi mtukufu wa Ramadhani ili tupate kuoanja utamu zaidi wa kumkurubia Mungu Muumba!
********
Mwenyezi Mungu anatuma salamu na kumswalia Mtume (saw) kutokana na imani yake thabiti, ikhlasi isiyo na mfano wake na juhudi yake kubwa katika njia ya Mwenyezi Mungu. Qur'ani Tukufu inatwambai kwamba Mwenyezi Mungu na Malaika wake daima wanatuma salamu na kumswalia Mtume Muhammad al-Mustafa (saw) na kututaka sisi waje wake pia tufanye vivyo hivyo. Aya ya 56 ya Surat al-Ahzab inabainisha suala hilo kwa njia ya kuvutia mno kwa kusema: "Hakika Mwenyezi Mungu na Malaika wake wanamsalia Nabii. Enyi mlioamini! Msalieni na mumsalimu kwa salamu (salimuni amri na kutii amri zake)." Kutuma salamu na kumswalia Mtume pamoja na Ahlu Bait wake watoharifu (as), si tu kwamba ni desturi bali ni jambo linaloonyesha upendo kwa mtu ambaye alitumia umri wake wote kwa ajili ya kuleta saada na kuwaongoza wanadamu kwenye njia nyoofu ya kutii amri na makatazo ya Muumba wao. Hivyo njooni tusome kwa pamoja na kwa sauti kubwa dhikri hii ya kuvutia: اللَّهُمَّ صَلِّ عَلَى مُحَمَّدٍ عَبْدِکَ وَ رَسُولِکَ، وَ أَهْلِ بَیْتِهِ الطَّاهِرِینَ
Allahumma Swalli Ala Muhammadin, Abdika wa Rasulika wa Ahli Baitihi at-Twahireen.
Dua ya siku ya 17 ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani inatuongoza kuelekea matendo mema kwa ibara na maneno yaliyojaa maana na ya kuvutia. Katika dua hii, tunamwomba Mwenyezi Mungu aziangaze nyoyo zetu katika mwezi huu uliojaa baraka kwa nuru ya wokovu na rehema zake. Inasema: "Ewe Mwenyezi Mungu! Katika siku hii niongoze kwenye kutenda mambo yanayofaa, nikidhie haja na matarajio yangu. Ewe ambaye hauhitajii kutafsiriwa wala kuulizwa! Ewe unayejua yaliyomo ndani ya nyoyo za walimwengu, Mswalie Muhammad na Ahli zake watoharifu!
Mwongozo wa Mweyezi Mungu unawahusu wanadamu wote. Kwa maana kuwa waumini na watu wasiokuwa na imani wakiwemo makafiri pia wanaweza kuongozwa na Mwenyezi Mungu. Ama waumini ni wale wanaochagua njia sahihi na kufanya juhudi za kupata ridhaa ya Mwenyezi Mungu maishani. Wacha-Mungu huwasadikisha Mitume wake ili wapate kufuata na kunufaika na mafundisho yao maishani. Mwenyezi Mungu pia huwapa thawabu maalum waumini na kuwatiisha kwa uongozi wake maalumu. Sio kwamba mtu anapoongoka huwa hawezi tena kupotea. Kwa hivyo, katika dua ya siku ya 17, tunaomba na kutoa moja ya matakwa yetu makuu kwa Mwenyezi Mungu kwa kusema: "Ewe Mwenyezi Mungu! Tuongoze kwenye matendo mema."
*********
Mafanikio ya kutenda mema ni mojawapo ya matakwa yetu muhimu katika dua ya siku hii. Tendo jema huambatanishwa na imani na hufanywa kwa nia ya kumkuribia Mwenyezi Mungu. Ibada, kuhiji, kusaidia masikini, kujenga zahanati na shule, kuamrisha mema na kukataza mabaya, kuwaongoza wajinga na kila jingine jema linalofanywa kwa ajili ya kupata ridhaa ya Mwenyezi Mungu ni mifano ya matendo mema. Hata kama jiwe litaanguka katikati ya njia wanakopita watu na mja akalisogeza kando ili lisitatize mapito ya watu, hili pia huchukuliwa kuwa ni jambo jema. Ni kama anavyosema Mwenyezi Mungu katika Aya ya 69 ya Surat al-Ankabut: "Na wanaofanya juhudi kwa ajili yetu, Sisi tutawaongoa kwenye njia zetu. Na hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja na watu wema."
Katika sehemu nyingine ya dua hii tunamwomba Mwenyezi Mungu atukidhie mahitaji na matarajio yetu. Matumaini ni kutaka kitu ambacho si rahisi kukipata, kiwe kinahitajika au la, ilhali haja ni kitu kinachohitajika na mwanadamu. Matumaini ni mojawapo ya sifa nzuri ambazo Mwenyezi Mungu ameziweka ndani ya maumbile ya mwanadamu na ndiyo humchochea mwanadamu kufanya harakati na kujitahidi maishani. Mtume (saw) anasema: "Matumaini na matarajio ni rehema kwa umma wangu, na kama hakungekuwepo matumaini, hakuna mama ambaye angemnyonyesha mtoto wake wala mtunza bustani kupanda mti."
Lakini matumaini na matamanio yanapovuka mipaka ya kawaida, humpoteza mtu na kumfanya azame katika mambo ya kidunia. Sawa kabisa na mvua ambayo ni rehema; lakini inapozidi na kupita viwango, hugeuka kuwa janga kubwa kwa kusababisha mafuriko. Mtukufu Mtume (saw) aliyachukulia "matumaini ya mbali na ya muda mrefu kuwa moja ya maadui wawili wakuu wa mwanadamu kwa kusema: "Kitu ambacho ninakichelea zaidi kwenu ni sifa mbili: Kufuata matakwa ya nafsi na matumaini marefu na ya mbali. Kuabudu matamanio hukuwekeni mbali na ukweli na matumaini ya mbali na ya muda mrefu hukufanyeni kuwa na pupa ya dunia." Kwa hiyo, katika sehemu hii ya dua, tunamwomba Mwenyezi Mungu Asiye Muhitaji atutimizie maombi yetu yote ambayo huimarisha ukuaji na ukamilifu wetu wa kibinadamu.
Mwishowe, tunamwomba Mungu kwa kusema: "Ewe Mwenyezi Mungu ambaye anajua kila kitu kilichoko ndani ya mioyo yetu na kile tunachokiamini, mawazo yetu yote mazuri na mabaya, na yote yaliyomo ndani ya mioyo ya walimwengu! Tunakuomba kwa unyenyekevu na kwa baraka za dua zinazojibiwa kutokana na kumswalia Muhammad na familia yake, tukidhie haja zetu zote."
Wapendwa wasikilizaji, na kufikia hapa ndipo tunafikia mwisho wa kipindi hiki cha 17 cha "Ramadhani, Mwezi wa Dhifa ya Mwenyezi Mungu. Tunatumai kimekuhimizeni muweze kutumia vyema baraka za mwezi huu mtukufu. Tunakuombeni mtenge wakati kwa ajili ya kunufaika na vipindi vinavyofuata tulivyokuandalieni kwa ajili ya mwezi huu mtukufu wa Ramadhani. Hadi wakati huo basi, jaribu kuwa karibu na Mwenyezi Mungu kwa kuomba na kutumia vizuri fursa za mwezi huu. Tunamwomba Mwenyezi Mungu atakabali amali zenu zote katika mwezi huu uliojaa baraka, kwaherini.