Ongezeko la askari wa Marekani nchini Afghanistan
https://parstoday.ir/sw/news/uncategorised-i40861-ongezeko_la_askari_wa_marekani_nchini_afghanistan
Kwa mujibu wa ripoti zilizotolewa, Marekani bado ina mpango wa kuongeza idadi ya askari wake nchini Afghanistan
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 25, 2018 23:09 UTC
  • Ongezeko la askari wa Marekani nchini Afghanistan

Kwa mujibu wa ripoti zilizotolewa, Marekani bado ina mpango wa kuongeza idadi ya askari wake nchini Afghanistan

Kwa mujibu wa John Nicholson, kamanda wa jeshi la Marekani na Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (NATO) aliyeko Afghanistan, zaidi ya askari 800 wengine wakiwemo washauri maalumu wa masuala ya kijeshi wa Marekani wanatazamiwa kutumwa nchini humo ndani ya wiki chache zijazo. Rais Donald Trump wa Marekani ametangaza stratijia mpya za kijeshi kwa ajili ya Afghanistan ambapo askari hao watasalia nchini humo kwa kipindi kisichojulikana kutokana na kile kinachotajwa na Washington kuwa ni mapambano dhidi ya kundi la Taleban.

Uvamizi wa Marekani nchini Afghanistan haujakuwa na faida yoyote kwa raia wa nchi hiyo ghairi ya kuwaletea vilio

Ni kwa ajili hiyo ndio maana Marekani katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita ikawa inaongeza idadi ya askari wake nchini Afghanistan kwa namna ya siri. Katika uwanja huo, kunaibuka maswali kadhaa kwamba, je, hivi ni kweli Washington inatuma askari zaidi nchini Afghanistan kwa ajili ya kupambana na makundi yanayotekeleza vitendo vya ukatili? Je, hadi sasa uwepo wa askari hao nchini humo umekuwa na mafanikio yoyote? Na ni nini lengo hasa la Marekani kuongeza idadi ya askari wake nchini Afghanistan? Itakumbukwa kuwa, Marekani iliivamia nchi hiyo mwaka 2001 kwa kisingizo cha kupambana na ugaidi ambapo katika uwanja huo ilitekeleza mauaji makubwa na hatimaye kuikalia kwa mabavu.

Licha ya Afghanistan kuelekea kuwa Vietnam ya pili kwa Marekani lakini bado Washington haijapata somo

Si tu kwamba Marekani imekuwa ikijishughulisha kupora vyanzo vya utajiri wa taifa hilo la Asia na pia kuhusika na biashara ya madawa ya kulevya, bali pia ili kufikia malengo yake mengine haramu katika eneo, imekuwa ikichochea makundi ya kigaidi na ya ukufurishaji katika eneo zima la Mashariki ya Kati. Kudhihiri kwa kundi la kigaidi la Daesh (ISIS) nchini Afghanistan na pia kusambaa ripoti zinazothibitisha kuhamishwa kwa helikopta za Marekani viongozi wa genge hilo, kumetimia katika uwanja huo. Ni kutokana na hali hiyo ndio maana Hamid Karzai, rais wa zamani wa nchi hiyo akasema: “Uwepo wa kijeshi wa Marekani nchini Afghanistan kwa karibu miongo miwili sasa, kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi, si tu kwamba haujasaidia hata kidogo kulitokomeza janga hilo, bali ndio kwanza umeimarisha wimbi la ugaidi.” Mwisho wa kunukuu.

Mauaji makubwa yanayoshuhudiwa kila siku nchini Afghanistan

Kabla ya mwaka 2014 na licha ya Marekani na Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (NATO) kuwa na askari wanaofikia laki moja na elfu 30 nchini Afghanistan hazikuweza kukabiliana na ugaidi, hivyo ni vipi Washington inadai kuwa itaweza kukanbiliana na tatizo hilo sugu nchini Afghanistan kwa kutumia askari karibu elfu 15 tu? Kwa msingi huo, tunaweza kusema kwamba, Marekani inafanya juhudi za kujiimarisha na kuboresha zaidi kambi zake za kjeshi katika maeneo tofauti ya Afghanistan. Hivyo kutumwa askari zaidi nchini humo pia kunafanyika kwa malengo ambayo yako mbali na maslahi ya Kabul, bali ni kwamba malengo hayo yanahatarisha usalama wa nchi hiyo na wa eneo zima kwa ujumla. Kuhusiana na suala hilo, Vahid Mojdeh, mtaalamu wa masuala ya kisiasa wa nchini Afghanistan anasema: “Malengo ya makundi ya kigaidi nchini Afghanistan ambayo kiuhalisia yanaungwa mkono na Marekani, ni kuibua matatizo kwa ajili ya nchi jirani ikiwemo China na mataifa ya Asia ya Kati.” Mwisho wa kunukuu.

Vahid Mojdeh, mtaalamu wa masuala ya kisiasa wa nchini Afghanistan

Alaa kullihaal, kuongezeka askari wa Marekani nchini Afghanistan kama nchi inayokaliwa kwa mabavu, ni kukariri tajriba iliyowahi kufeli nchini humo kwa zaidi ya miaka 100 iliyopita ambayo ilifanywa na jeshi la Uingereza na kadhalika Urusi ya zamani, ambapo raia wa Afghanistan walionyesha kwamba, kamwe hawakubaliani na aina yoyote ya uvamizi dhidi ya nchi yao. Suala ambalo hivi karibuni pia liliashiriwa na Mohammad Ismail Khan, kiongozi wa zamani wa harakati ya jihadi ambaye aliionya Marekani kwamba inatakiwa kukumbuka hatma mbaya ya wavamizi wa taifa hilo waliotangulia. Kama ambavyo mwaka 2014 rais wa zamani wa Marekani Barack Obama kwa kuhofia kubadilika Afghanistan kuwa Vietnam nyingine kwa Marekani, alilazimika kuondoa idadi kubwa ya askari wa nchi yake kutoka Afghanistan. Hata hivyo kile ambacho kinaonekana kwa Rais wa sasa Donald Trump ni kutopata somo na ibra juu ya matukio yaliyowahi kujiri nchini Afghanistan na hatma ya wavamizi wa nchi hiyo.