Utayarifu wa China wa kusaidia kustawisha uchumi wa Korea Kaskazini
Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi amesema kuwa, Beijing itaisaidia Korea kaskazini katika kukuza uchumi na ustawi wa nchi hiyo.
Wang Yi ameyasema hayo kando na kikao cha muungano wa Association of Southeast Asian Nations kwa kifupi ASEAN kilichofanyika nchini Singapore wakati alipokutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea Kaskazini na kusisitiza kuwa, China imeandaa misaada yake ya lazima kwa ajili ya kustawisha uchumi wa nchi hiyo. Kwa upande wake Ri Yong-ho, Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea Kaskazini amesema, Pyongyang inataka kushirikiana na China kwa ajili ya kudhamini usalama na uthabiti endelevu katika Rasi ya Korea. Sambamba na kuonyesha matarajio yake kwa ajili ya kufungamana Pyongyang na majukumu yake, Waziri wa Mambo ya Nje wa China amesema kuwa, Marekani inatakiwa izingatie wasi wasi ilionao Korea Kaskazini. Akizungumzia wasi wasi ilionao Pyongyang juu ya uvunjaji ahadi wa Marekani, Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea Kaskazini, amesema kuwa nchi yake imefungamana na majukumu yake kwa ajili ya kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa na Marekani mwezi Juni uliopita, na kusisitiza kuwa, Korea Kaskazini bado ina wasi wasi juu ya miamala hasi ya White House kuhusiana na suala hilo.
Hatua ya China ya kutangaza utayarifu wake kwa ajili ya kusaidia kuinua na kustawisha uchumi wa Korea Kaskazini, imekuja ikiwa ni baada ya mazungumzo kati ya Kim Jong-un na Donald Trump yaliyofanyika nchini Singapore mwezi Juni mwaka huu, suala ambalo lilileta matumaini katika ngazi ya kimataifa hususan kati ya nchi zenye mzozo za ukanda wa Korea ikiwemo China juu ya kupungua mzozo huo hasa baada ya kuboreka mahusiano kati ya Pyongyang na Washington. Kwa mtazamo wa China, kuendelea mzozo katika uhusiano wa Marekani na Korea Kaskazini, ambao utapelekea kuvurugika uthabiti na usalama kupitia hatua za uchochezi za White House ndani ya eneo la Korea, utasababisha taathira hasi kwenye ukuaji uchumi hata kwa China pia. Ni kwa ajili hiyo ndio maana Beijing ikakaribisha mwenendo ulioanza kupitia fremu ya mazungumzo kati ya Marekani na Korea Kaskazini kwa ajili ya kutatua tofauti za pande mbili na kusema kuwa hatua hiyo ni yenye taathira chanya katika eneo. Hata hivyo baada ya China kuwashawishi viongozi wa Marekani na Korea Kaskazini kutatua mzozo kupitia njia ya udiplomasia na mazungumzo, bado ina wasi wasi juu ya hali ya mambo katika eneo baada ya kutatuliwa mzozo huo. Moja ya wasi wasi ilionao China katika uwanja huo ni stratijia ya Marekani kwa ajili ya kuitenganisha Korea Kaskazini na Beijing sambamba na kuyafanya mahusiano ya nchi mbili kuwa dhaifu zaidi, kupitia kuboreshwa mahusiano mapya kati ya Pyongyang na Washington.
Katika hali hiyo, inachopendelea China na kuona kinatendeka katika mwenendo wa mazungumzo kati ya Marekani na Korea Kaskazini ni kutiwa saini makubaliano ya amani ambayo yatahitimisha vita na uhasama katika eneo hilo sambamba na kuondolewa karibu askari elfu 28 wa Marekani kutoka Korea Kusini. Kufikiwa makubaliano kama hayo kati ya Pyongyang na Washington, kutapelekea kuandaliwa anga nzuri kwa China kuweza kupenya zaidi nchini Korea Kaskazini. Hata hivyo China inaamini kuwa ni suala lililo mbali kufanyika mabadiliko ya kweli katika siasa za kigeni za Korea Kaskazini kuelekea harakati za sera chanya za kujitegemea chini ya ushirikiano na Marekani. Lakini wasi wasi ilionao Beijing ni kwamba Washington inafanya juu chini kuhakikisha inaharibu ushirikiano kati ya China na Korea Kaskazini. Ni katika mahesabu hayo ndipo Waziri wa Mambo ya Nje wa China akatangaza utayarifu wa nchi yake wa kushirikiana zaidi na Korea Kaskazini kwa ajili ya kustawisha uchumi wa nchi hiyo.