Hujuma ya kigaidi msikitini Afghanistan, wanne wauawa
https://parstoday.ir/sw/news/uncategorised-i8914-hujuma_ya_kigaidi_msikitini_afghanistan_wanne_wauawa
Watu wanne wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa wakati magaidi walipoulenga msikiti kwa bomu katika mkoa wa Nangarhar mashariki mwa Afghanistan.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 10, 2016 23:16 UTC
  • Hujuma ya kigaidi msikitini Afghanistan, wanne wauawa

Watu wanne wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa wakati magaidi walipoulenga msikiti kwa bomu katika mkoa wa Nangarhar mashariki mwa Afghanistan.

Imearifiwa kuwa mlipuko huo umejiri baad aya Sala ya Ijumaa katika Msikiti wa Jamia wa Hisarak katika wilaya ya Rodat yapata kilomita 120 magharibi mwa mji mkuu Kabul.

Ataullah Khogyani, msemaji wa mkuu wa mkoa wa Nangarhar amesema Imamu wa msikiti ni kati ya waliouawa na kwamba watu wengine 40 wamejeruhiwa.

Amebainisha wasiwasi wake kuwa yamkini idadi ya waliopoteza maisha ikaongezeka kutokana na kuwa baadhi ya waliojeruhiwa wako katika hali mahututi.

Hakuna kundi lolote lililodai kuhusika na hujuma hiyo lakini duru za usalama zinayashuku makundi ya kigaidi ya Taliban na ISIS au Daesh kuwa yamehusika.

Serikali ya Afghanistan hivi karibuni ilitangaza kusambaratisha ngome kuu ya kundi la kigaidi na kitakfiri la ISIS katika wilaya ya Achin mkoani Nangarhar.