Jul 20, 2023 07:33 UTC
  • Kuvunjiwa heshima Qurani; Wairaq waushambulia ubalozi wa Sweden

Wananchi wa Iraq waliokuwa na ghadhabu wameuvamia ubalozi wa Sweden mjini Baghdad na kuchoma moto sehemu moja ya ofisi za ubalozi huo, kulalamikia kibali cha pili kilichotolewa na serikali ya Stockholm cha kuruhusu kuvunjiwa heshima Qurani Tukufu katika nchi hiyo ya Ulaya.

Waandamanaji hao ambao akthari yao ni wafuasi wa Muqtada al-Sadr, Kiongozi wa Harakati ya Al-Sadr ya nchini Iraq mapema leo Alkhamisi wameshambulia malango ya jengo la ubalozi huo wa Sweden mjini Baghdad huku wakiwa wamebeba Misahafu.

Wamesikika wakipiga nara za kulaani vitendo vya kuvunjiwa heshima Qurani Tukufu nchini Sweden kwa ridhaa ya serikali. Wizara ya Mambo ya Nje ya Iraq imewakosoa waandamanaji hao ikisisitiza kuwa, maafisa wote wa ubalozi huo wako salama.

Sweden imebariki kuvunjiwa heshima Qurani Tukufu kwa mara nyingine tena, licha ya Waziri wa Sheria wa nchi hiyo hivi karibuni kukiri hadharani madhara ya kiusalama ya kuvunjiwa heshima matukufu ya kidini nchini humo, na akatangaza kwamba sasa serikali ya nchi hiyo imeamua kuchunguza uwezekano wa kuharamisha na kupiga marufuku kuchomwa moto Kitabu hicho kitukufu cha Waislamu.

Ikumbukwe kuwa, Juni 28, Mswidi Salwan Momika mwenye umri wa miaka 37, alichoma moto nakala ya Qur'ani Tukufu mbele ya Msikiti mkuu wa Stockholm, siku ambayo Waislamu Sweden walikuwa katika siku ya kwanza ya Idul Adh’ha.

Mkimbizi huyo wa Iraq aliyepewa uraia wa Sweden alikivunjia heshima Kitabu kitakatifu cha Waislamu bilioni mbili kwa kibali cha mahakama ya Sweden na kwa ulinzi kamili wa jeshi la polisi la nchi hiyo ya Ulaya Magharibi.

Waislamu kote duniani wameendelea kupaza sauti zao kulaani kitendo hicho kiovu cha kudhalilisha na kuvunjiwa heshima Qurani Tukufu nchini Sweden, huku kampeni kubwa ya dunia nzima ya kususia bidhaa zinazozalishwa na nchi hiyo ya Magharibi ikishika kasi.

Tags