Sababu za Marekani kurudisha kundi la kigaidi la Daesh nchini Syria
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i101238-sababu_za_marekani_kurudisha_kundi_la_kigaidi_la_daesh_nchini_syria
Kundi la kigaidi la Daesh au jina jingine ISIS, limezidisha mashambulizi yake katika ardhi ya Syria. Syria na Iran zimeshuhudia mashambulizi ya kigaidi ya kundi hilo katika wiki za hivi karibuni. Kuna dalili za kutosha zinazothibitisha kwamba Marekani ndiyo inayochochea mashambulizi hayo.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Aug 19, 2023 04:48 UTC
  • Sababu za Marekani kurudisha kundi la kigaidi la Daesh nchini Syria

Kundi la kigaidi la Daesh au jina jingine ISIS, limezidisha mashambulizi yake katika ardhi ya Syria. Syria na Iran zimeshuhudia mashambulizi ya kigaidi ya kundi hilo katika wiki za hivi karibuni. Kuna dalili za kutosha zinazothibitisha kwamba Marekani ndiyo inayochochea mashambulizi hayo.

Shirika la habari la Associated Press limesema katika ripoti kwamba kundi la wataalamu wa Umoja wa Mataifa limesema katika ripoti kwa Baraza la umoja huo kwamba katika nusu ya kwanza ya mwaka huu, tishio la Daesh limeongezeka katika baadhi ya maeneo yenye migogoro huko Iraq na Syria. Kwa mujibu wa shirika hilo la habari, ripoti ya wataalamu hao inasema licha ya Daesh kupata hasara na maafa makubwa katika shughuli zake katika nchi za Syria na Iraq na kupungua operesheni zake za kigaidi katika nchi hizo, lakini bado kuna hatari ya kuimarika tena. Seyyed Hassan Nasrallah, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon hivi karibuni alisema: "Marekani imeamua kulirejesha tena uwanjani kundi la kigaidi la Daesh." Je, ni kwanini Marekani imechukua uamuzi wa kuhuisha na kulirejesha tena kundi hilo la kigaidi katika matukio ya Asia Magharibi?

Baadhi ya wanachama wa kundi hilo nchini Syria wako katika kambi ambazo baadhi ziko chini ya udhibiti wa Marekani. Kambi ya al-Hol katika jimbo la al-Hasaka, ambalo ni kituo kikuu cha kuzuiliwa magaidi wa ISIS, ni mojawapo ya kambi hizo. Hadi sasa vyanzo vingi vya ndani vimeripoti kuwa jeshi la Marekani linawahamisha magaidi wa ISIS kutoka magerezani na kuwapeleka katika kambi za kijeshi, ambapo vyanzo vya usalama vimekuwa vikisema mara kwa mara kwamba Marekani inawafunza na kuwapa zana za kijeshi ili kutekeleza mashambulizi ya kigaidi nchini Syria, na hicho kuwa kisingizio cha nchi hiyo kuendelea kuwepo kijeshi katika ardhi ya Syria.

Magaidi wa Daesh wakiwa kizuizini

Kwa hakika Wamarekani ambao wako chini ya mashinikizo ya wananchi wa Syria kwa ajili ya kuliondoa jeshi la nchi hiyo katika ardhi yao, wanaona kuendelea jinai za Daesh kuwa kunadhamini maslahi yao ya kuendelea kubakia katika nchi hiyo ya Kiarabu.

Kuhusu suala hilo, Khayyam al-Zu'bi, mwandishi wa Syria, amechapisha makala katika gazeti la elektroniki la Rai' Alyoum, akiashiria malengo ya harakati za Marekani na kutumia tena chombo cha magaidi wa Daesh na kusema: "Matukio yaliyotokea kaskazini na mashariki mwa Syria, ambayo yako nje ya udhibiti wa serikali ya Syria, kwa hakika ni kwa manufaa ya Marekani. Washington inataka kukosekana utulivu na usalama nchini Syria, na inafuatilia kwa karibu suala hilo kupitia uungaji mkono kwa makundi ya kigaidi na yanayotaka kujitenga nchini humo."

Mbali na kuendelea kuiweka Syria katika hali ya ghasia na udhaifu, Marekani pia inafuatilia njama za kuziwekea mashinikizo nchi za Iran na Russia nchini Syria kupitia juhudi za kuwarejesha magaidi wa Daesh katika ardhi ya Syria. Lengo jingine la Marekani ni kuzuia kuanzishwa njia ya mawasiliano kati ya Iran, Iraq na Syria. Katika muktadha huu, James Jeffrey, mjumbe wa zamani wa Marekani nchini Syria, anasema kwamba majeshi ya nchi hiyo hayataondoka Syria. Anasisitiza kwa kusema: "Tupo al-Tanaf ili kukata njia kuu ya mawasiliano kati ya Damascus na Tehran kusini mwa Syria." Wakati wa utawala wa Donald Trump pia juhudi kubwa zilifanywa na watawala wa Marekani ili kuongeza mashinikizo dhidi ya serikali ya Rais Bashar al-Assad wa Syria.