Kambi za kijeshi za Marekani zashambuliwa kwa droni Iraq, Syria
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i104314-kambi_za_kijeshi_za_marekani_zashambuliwa_kwa_droni_iraq_syria
Vituo viwili vya kijeshi vya Marekani vimeshambuliwa katika hujuma za ndege zisizo na rubani (droni) katika eneo la Kurdistan la kaskazini mwa Iraq na katika mkoa wa Hasaka, mashariki mwa Syria.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Nov 04, 2023 03:03 UTC
  • Kambi za kijeshi za Marekani zashambuliwa kwa droni Iraq, Syria

Vituo viwili vya kijeshi vya Marekani vimeshambuliwa katika hujuma za ndege zisizo na rubani (droni) katika eneo la Kurdistan la kaskazini mwa Iraq na katika mkoa wa Hasaka, mashariki mwa Syria.

Kambi hizo za Marekani zimeshambuliwa kwa droni katika wimbi jipya la mashambulizi ya makundi ya muqawama dhidi ya vikosi hivyo vamizi katika nchi jirani za Iraq na Syria.

Duru za habari zinaarifu kuwa, kambi ya kijeshi ya Marekani karibu na Uwanja wa Kimataifa wa Ndege mjini Erbil, huko Kurdistan ya Iraq ilishambuliwa jana Ijumaa kwa droni na Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Iraq, ambayo ni sehemu ya makundi yanayopambana na ugaidi nchini humo.

Kundi hilo la muqawama limetangaza kuhusika na shambulio hilo katika taarifa iliyochapishwa kwenye chaneli yake yake ya Telegram na kuongeza kuwa, limeshambulia kambi hiyo ya US kwa kutumia droni mbili, kutokana na hatua ya Washington ya kuunga mkono hujuma za kikatili za Israel dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza. 

Kambi ya kijeshi ya Marekani mjini Erbil

Msemaji wa Pentagon, Brigedia Jenerali Pat Ryder amethibitisha habari hizo za kushambuliwa wanajeshi wa Marekani katika mji wa Erbil kaskazini mwa Iraq.

Habari zaidi zinasema kuwa, kituo cha kijeshi cha Marekani cha Ash Shaddadi katika mkoa wa Hasaka mashariki mwa Syria kilishambuliwa jana pia na wanamuqawama wa nchi hiyo ya Kiarabu.

Pentagon imesema kambi za kijeshi za Marekani zimeshambuliwa angalau mara 16 kwa droni na maroketi katika nchi za Iraq na Syria, baina ya Oktoba 17 na 26, kabla ya hujuma hizo za droni za jana Ijumaa.