Hatimaye vita vya Gaza vyasimamishwa kwa muda wa siku 4
(last modified Wed, 22 Nov 2023 06:39:27 GMT )
Nov 22, 2023 06:39 UTC
  • Hatimaye vita vya Gaza vyasimamishwa kwa muda wa siku 4

Hatimaye kumefikiwa makubaliano ya kusitisha vita huko Gaza kwa muda wa siku nne ili kutoa fursa ya kufikishwa misaada ya kibinadamu na pande mbili kubadilishana mateka.

Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina "Hamas" imeitangaza katika taarifa yake kwamba, baada ya mazungumzo magumu na tata na marefu, tunatangaza kwamba kwa msaada wa Mwenyezi Mungu na juhudi kubwa za Qatar na Misri, tumefikia makubaliano ya kibinadamu ya kusitisha mapigano (ya muda mfupi) kwa muda wa siku 4.

Katika muendelezo wa taarifa yake, harakati ya Hamas iimebainisha vipengee vya makubaliano hayo, ambayo kwa mujibu wake, mapigano ya pande zote mbili, shughuli za kijeshi za jeshi la Kizayuni katika maeneo yote ya Gaza, na harakati za magari ya kivita ya utawala huo huko Ghaza zitasimamishwa.

Wapalestina zaidi ya 14,000 wameuawa shahidi tangu Israel ilipoanzisha mashambulio yake ya kinyama katika Ukanda wa Gaza ikiwa ni radiamali yake ya operesheni ya Kimbunga cha al-Aqswa

 

Kwa mujibu wa makubaliano hayo, mamia ya malori maalumu yaliyobeba misaada ya kibinadamu, misaada ya matibabu na mafuta yataingia katika maeneo yote ya Gaza bila pingamizi.

Aidha taarifa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imeeleza kuwa, anawake na watoto 50 wa Israel walio chini ya umri wa miaka 19 wataachiliwa huru mkabala wa wanawake na watoto 150 wa Kipalestina walio chini ya umri wa miaka 19 kwa kuzingatia rekodi za mateka.

Hamas imesisitiza kuwa katika kipindi cha usitishaji vita, utawala unaokalia kwa mabavu umeahidi kutoshambulia au kufanya hujuma dhidi ya mtu yeyote katika maeneo yote ya Ukanda wa Gaza, na watu watakuwa na uhuru wa kuvuka kutoka kaskazini mwa Gaza kuelekea kusini kkatika barabara Mtaa wa Salah al-Din.