Makubaliano ya kusitisha vita Gaza yarefushwa kwa siku 2 zaidi
(last modified Tue, 28 Nov 2023 07:12:19 GMT )
Nov 28, 2023 07:12 UTC
  • Makubaliano ya kusitisha vita  Gaza yarefushwa kwa siku 2 zaidi

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Qatar na Harakati ya Hamas zimetangaza kuwa, makubaliano ya usitishaji vita huko Gaza yameongezwa muda kwa siku mbili zaidi, kwa msingi wa masharti yale yale ya awali.

Kwa mujibu wa ripoti ya shirika la habari la Fars Jumatatu, baada ya kumalizika usitishaji vita wa siku nne, Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar imetangaza kuwa usitishaji mapigano  huko Gaza umeongezwa muda wa siku mbili zaidi.

Huku ikithibitisha makubaliano hayo, harakati ya Hamas imesema: Tumekubaliana na ndugu zetu wa Misri na Qatar juu ya kurefushwa kwa muda usitishaji vita kwa siku nyingine mbili kwa masharti yale yale ya awali.

Majed bin Mohammad Al-Ansari, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar, amesisitiza kwamba juhudi za kurefusha usitishaji vita wa kibinadamu katika Ukanda wa Gaza bado zinaendelea na kusema: 'Madhumuni ya kurefushwa muda wa usitishaji vita ni kufikishwa misaada na kuachiliwa wafungwa na mateka. Tumepokea ujumbe kutoka upande wa pili kwa ajili ya kurefusha muda wa usitishaji mapigano.'

Al-Ansari pia ameelezea matumaini yake kuwa usitishaji vita huo utapelekea kumalizika mzozo kati ya makundi ya muqawama wa Palestina na utawala wa Kizayuni.

 

Inafaa kuashiria hapa kuwa usitishaji vita wa siku 4 ulianza kutekelezwa asubuhi ya Ijumaa ya tarehe 24 Novemba ikiwa ni baada ya siku 49 za mapigano kati ya harakati ya mapambano ya Kiislamu ya Hamas na utawala wa Kizayuni huko Gaza.

Hamu ya utawala ghasibu wa Israel ya kurefusha muda wa usitishaji vita huko Gaza inakuja wakati ambapo wataalamu hata ndani ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu (Israel) wanatilia shaka uwezo na nguvu ya utawala huo kufanikiwa kufikia malengo yake ya vita huko Gaza.

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, tarehe 7 Oktoba ilianzisha operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu kutokea Gaza ili kukabiliana na zaidi ya miongo saba ya kukaliwa kwa mabavu Palestina na takriban miongo miwili ya kuzingirwa Ukanda wa Gaza pamoja na kufungwa jela na kuteswa maelfu ya Wapalestina.

Operesheni hiyo ilikuwa moja ya mashambulizi makubwa zaidi kuwahi kufanyika dhidi ya utawala huo wa Kizayuni.

Katika kukabiliana na operesheni hiyo, utawala wa Kizayuni umetekeleza mashambulizi ya kikatili dhidi ya Gaza na kuliweka eneo hilo chini ya mzingiro kamili. Mashambulio hayo yamepelekea zaidi ya raia 14,500 kuuawa shahidi.