Israel yazidisha ukatili dhidi ya Wapalestina kwa himaya ya Marekani
Ripoti za hivi karibuni zinaonesha kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel umezidisha ukandamizaji na ukatili dhidi ya watu wanaoendelea kukandamizwa wa Palestina.
Kamati inayoshughulikia masuala ya mateka wa Palestina katika korokoro za Israel imetangaza kuwa, katika kipindi cha miezi sita ya kwanza ya mwaka huu wa 2016 utawala haramu wa Israel umewatia nguvuni Wapalestina 3445 katika maeneo mbalimbali yanayokaliwa kwa mabavu. Takwimu hizo zinaonesha kuwa, wastani wa kutiwa nguvuni Wapalestina katika mwaka huu umeongezeka kwa asilimia 50 ikilinganishwa na mwaka uliopita.
Kwa sasa zaidi ya Wapalestina 7500 wanashikiliwa katika korokoro za kutisha za Israel.
Mwenendo huo wa kuzidisha ukandamizaji dhidi ya raia wa Palestina unaendelezwa na Israel huku Marekani ikitangaza kuwa iko tayari kuzidisha misaada yake ya kila mwaka kwa utawala huo ghasibu. Susan Rice ambaye ni Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Rais wa Marekani amesema kuwa White House imeitumia barua Congresi ya nchi hiyo ikitangaza kuwa iko tayari kuzidisha misaada ya kijeshi kwa utawala wa Kizayuni wa Israel baada ya kumalizika muda wa makubaliano ya misaada ya sasa hapo mwaka 2018. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, utawala wa Kizayuni wa Israel unapewa dola bilioni tatu kila mwaka. Lakini kwa mujibu wa makubalino mapya ambayo yatatekelezwa kwa kipindi cha miaka 10, Israel itapewa misaada kikubwa zaidi ya kijeshi ya Marekani inayotolewa kwa nchi au upande wowote wa kigeni. Msaada huo unaambatana na uhuru wa kutumiwa popote na kwa sababu yoyote ile.
Israel inataka kuzidishwa msaada huo na kuwa dola bilioni 42 hadi 45 hadi kufikia mwaka 2018.
Gazeti la The Times of Israel limefichua kuwa, kwa sasa maafisa wa utawala huo wameiomba Marekani izidishe misaada yake ya kila mwaka kwa utawala huo.
Marekani imekuwa ikitaka kuzidisha uwezo wa utawala wa Kizayuni na katili wa Israel kwa kutumia mbinu mbalimbali na mwenendo huo unatambuliwa kuwa ni ruhusa ya Washington na baraka zake kwa jinai zote zinazoendelea kufanywa na utawala huo dhidi ya raia wanaodhulumiwa wa Palestina. Washington ambayo ndiye mshirika mkubwa zaidi wa Israel, imekuwa ikiufadhili na kuusaidia utawala huo bandia kwa hali na mali tangu ulipoundwa katika ardhi ya Palestina.
Ombi la kuzidishwa misaada ya Marekani kwa Israel limetolewa wakati Barack Obama pia akifanya mikakati ya kulishawishi kundi la mashinikizo la Wazayuni nchini Marekani AIPAC kwa ajili ya kupata uungaji mkono wao kwa chama chake cha Democratic katika uchaguzi ujao wa rais.
Historia ya uhusiano wa Marekani na Israel inaonesha kuwa, suala la kulindwa uhusiano huo linapewa nafasi maalumu katika siasa za nje za Marekani, na Washington haiko tayari kubadili msimamo huo kwa hali yoyote ile.
Alaa kulli hal, misaada ya Marekani kwa utawala katili wa Israel inautia kiburi zaidi utawala huo kwa ajili ya kudumisha na kuzidisha unyama na kutenda jinai dhidi ya watu wa Palestina na kuhatarisha amani ya kimataifa.