Njama za Marekani za kuendelea kubakia kijeshi nchini Iraq
(last modified Thu, 11 Jan 2024 07:14:41 GMT )
Jan 11, 2024 07:14 UTC
  • Njama za Marekani za kuendelea kubakia kijeshi nchini Iraq

Licha ya serikali ya Iraq kuitaka Marekani iondoe wanajeshi wake nchini humo, lakini Washington imetangaza kuwa, haina ratiba yoyote ya kutoka katika nchi hiyo ya Kiarabu.

Patrick Ryder, msemaji wa wizara ya ulinzi ya Marekani, Pentagon, amesema kuwa, nchi hiyo haina mpango wa kuwaondoa wanajeshi wake walioko nchini Iraq kwa kile alichodai kuwa, bado inaendelea kupambana na genge la kigaidi la DAESH (ISIS). Amedai kuwa, Marekani iko Iraq kiushauri wa kiusalama na eti wanaisaidia serikali ya Iraq kupambana na magaidi. 

Hii ni katika hali ambayo, Waziri Mkuu wa Iraq, Mohammed Shia' Al Sudani amesema wakati wa kumbukumbu ya mwaka wa nne wa kuuawa shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) na Shahid Abu Mahdi al Muhandis, aliyekuwa Naibu wa Harakati ya Hashd al Shaabi ya Iraq kwamba, msimamo usiotetereka na wa kimsingi wa serikali ya Iraq ni kuondoka wanajeshi wa kigeni nchini humo kwani hakuna kisingizio na sababu nyingine yoyote ya kubakia nchini humo.

sl

Marekani inafanya wizi mkubwa wa mafuta katika nchi za Iraq na Syria

 

Amesisitiza kuwa, hatua yoyote ya kukanyaga na kutoheshimu haki ya kujitawala Iraq inapingwa vikali na serikali yake na hayo ndiyo mambo ambayo yanaifanya mara kwa mara Baghdad kusisitizia wajibu wa kutoka askari wa kigeni nchini humo.

Kwa zaidi ya miaka 20 sasa Marekani inang'ang'ania kubakia kijeshi huko Iraq na mpaka leo viongozi wa Washington wanadai kuwa eti wanapambana na ugaidi. Hayo yanatendeka wakati ambapo katika uhalisia wa mambo, uvamizi wa kijeshi wa Marekani nchini Iraq ndio uliotanua vitendo vya kigaidi nchini humo kiasi kwamba, baada ya Marekani kuivamia kijeshi Iraq, nchi hiyo imepitisha kipindi kirefu cha ukosefu wa amani. Magenge ya kigaidi na ukufurishaji hasa Daesh (ISIS) na ambayo yameundwa na hilo hilo dola la kiistikbari la Marekani, yalifikia hata kuteka eneo kubwa la Iraq na kutangaza serikali yao ndani ya nchi hiyo na nchi jirani ya Syria. 

Kwa kweli tofauti na inavyodai Marekani, Washington haiwezi kabisa kukanusha nafasi yake kubwa katika kuundika genge la kigaidi la Daesh na kupata nguvu katika nchi za Iraq na Syria. Magaidi kutoka kona mbalimbali za dunia hasa nchi za Magharibi walikusanyika pamoja katika baadhi ya maeneo ya Iraq wakati nchi hiyo ilipokuwa imevamiwa na madola vamizi ya Marekani na Uingereza. Baada ya hapo na kwa ajili ya kupotosha fikra za walio wengi duniani, madola hayo ya Magharibi yalijifanya kuunda muungano wa eti kupambana na ugaidi wa Daesh. Hadi hivi sasa kisingizio hicho hicho ndicho kinachotumiwa na Marekani kung'ang'ania kubakia kijeshi nchini Iraq.

Patrick Ryder

 

Alaakullihaal, katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, serikali ya Iraq imezidisha mashinikizo ya kuitaka Marekani iondoke kijeshi nchini humo kwani kuwepo kwake kunazidisha tu vitendo vya kigaidi, kunaifisidi kiuchumi Iraq, na vilevile Washington inazidi kupora utajiri wa nchi hiyo na nchi jirani ya Syria, haiheshimu uhuru wa kujitawala nchi hizo na pia inaingilia waziwazi masuala ya ndani ya nchi hizo. 

Serikali ya hivi sasa ya Marekani inaendelea kushikilia kubakia kijeshi nchini Iraq katika hali ambayo viongozi wengi tu wa Washington wamekuwa wakikiri mara kwa mara kuhusu kosa la kuendelea kuweko wanajeshi wa Marekani huko Iraq na wamekuwa wakiihimiza White House ikiri kushindwa na iondoke nchini humo, lakini viongozi ving'ang'anizi wa dola hilo la kibeberu wanaendelea kufanya ukaidi. 

Inavyoonekana wazi ni kwamba Marekani si tu haiko tayari kuondoka nchini Iraq, lakini pia inatumia njia mbalimbali za kuishinikiza serikali ya Baghdad yakiwemo mashinikizo ya kiuchumi na kuchochea machafuko ili amani na usalama usipatikane kabisa nchini humo na hicho kiwe kisingizio cha kuendelea kubakia wanajeshi vamizi wa Marekani katika nchi hiyo ya Kiarabu.

Tags