Ansarullah: Marekani na Uingereza zijiandae 'kulipa gharama kubwa' kwa kuishambulia Yemen
(last modified Fri, 12 Jan 2024 07:44:19 GMT )
Jan 12, 2024 07:44 UTC
  • Ansarullah: Marekani na Uingereza zijiandae 'kulipa gharama kubwa' kwa kuishambulia Yemen

Harakati ya Muqawama ya Ansarullah ya Yemen imezilaani vikali Marekani na Uingereza baada ya kufanya mashambulizi makali dhidi ya vituo vyake ndani ya Yemen, na kuonya kuwa vituo vya kijeshi vya nchi hizo vilivyoko katika eneo vitashambuliwa iwapo zitafanya uchokozi zaidi.

Mashambulizi dhidi ya Yemen yamefanywa baada ya vikosi vya nchi hiyo kuzishambulia meli kadhaa zinazomilikiwa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika Bahari Nyekundu, ikiwa ni hatua ya kuwaunga mkono Wapalestina wa Gaza wanaoandamwa na vita vya mauaji ya kimbari na ya halaiki vinavyoendeshwa na utawala huo wa Kizayuni, ambapo zaidi ya Wapalestina 23,000 wameshauawa shahidi na wengine wapatao 60,000 wamejeruhiwa hadi sasa katika mashambulizi hayo ya Israel yaliyoanza Oktoba 7.

Akizunngumza na televisheni ya Aljazeera ya Qatar mapema leo, Naibu Mkurugenzi wa Idara ya Mwongozo wa Maadili ya Ansarullah, Brigedia Jenerali Abdullah bin Amer amesema: Washington na London lazima zikubali kubeba dhima ya kuvuruga hali ya mambo katika Bahari Nyekundu, na kulifanya eneo hilo la majini kuwa la harakati za kijeshi.

Jenerali Bin Amer amesisitiza kuwa, ni lazima Marekani na Uingereza zijiweke tayari  kulipa gharama kubwa, na kukabiliana na matokeo mabaya ya uchokozi wa waziwazi ziliofanya.

Ameongezea kwa kusema, "Sisi (Vikosi vya Wanajeshi wa Yemen) tutavishambulia vituo vyao katika eneo ikiwa Marekani na Uingereza zitaongeza mashambulizi yao [dhidi ya Yemen]."

Bin Amer amebainisha kuwa miripuko imeripotiwa katika miji kadhaa nchini Yemen, ukiwemo mji mkuu Sana’a na mji wa bandari wa al-Hudaydah, na kusisitiza kwamba vikosi vya Yemen vitajibu kwa nguvu vitendo hivyo vya uchokozi.

"Tutaendelea na operesheni zetu katika Bahari Nyekundu hadi uvamizi [wa Israel] dhidi ya Gaza ukomeshwe,"amesisitiza kwa mara nyingine afisa huyo mwandamizi wa Ansarullah.

Mapema leo, vikosi vya Marekani na Uingereza vilianzisha mashambulizi ya anga na ya kutumia manowari na nyambizi dhidi ya maeneo kadhaa ndani ya Yemen.../