Hizbullah yazima uvamizi wa kijeshi wa Israel kusini ya Lebanon
Wanajihadi wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon wametibua uvamizi wa kijeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel kusini mwa nchi hiyo ya Kiarabu, huku ngome za utawala huo ghasibu zikiendelea kulengwa kwa makombora ya kundi hilo la muqawama, likiwa ni jibu kwa mauaji ya kimbari yanayoendelea kufanywa na Wazayuni katika Ukanda wa Gaza.
Kanali ya televisheni ya al-Manar ya Lebanon imetangaza kuwa, wanamuqawama hao wa Hizbullah wamelishambulia na kulisababishia hasara kubwa jeshi la utawala wa Kizayuni katika mji wa Zar'it karibu na mpaka wa Lebanon, lilipokuwa likijiandaa kushambulia maeneo ya kusini mwa Lebanon.
Al-Manar imenukuu taarifa ya Hizbullah inayosema kuwa, wanajeshi kadhaa wa utawala wa Kizayuni wamejeruhiwa kwenye makabiliano na wanamuqawama mapema leo Jumatatu.
Haya yanajiri saa chache baada ya Hizbullah kusema katika taarifa kuwa, wapambanaji wake washambulia kwa kombora zito la Burkan mkusanyiko wa wanajeshi wa Israel katika kituo cha Hadab al-Bustan.
Al-Manar imeripoti kuwa, wanajeshi kadhaa wa Kizayuni wameangamizwa na kujeruhiwa kwenye shambulio hilo la kombora la jana jioni la Hizbullah.
Sambamba na hayo, Harakati ya Hizbullah ya Lebanon pia inaendelea kukabiliana na adui Mzayuni kaskazini mwa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na kutoa vipigo kwa utawala ghasibu kwa kuvishambulia vituo vyake vya kijeshi, ujasusi na zana za kijeshi.
Hivi karibuni, Avikhai Adrei, msemaji wa jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel alikiri kuwa, mashambulizi ya makombora ya Harakati ya Hizbullah ya Lebanon huko Kefriwal, kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu (Israel) yamekwua na ufanisi na kulenga shabaha.