Jan 25, 2024 03:27 UTC
  • Yahya Rasoul
    Yahya Rasoul

Msemaji wa Amiri Jeshi Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Iraq amelaani mashambulizi ya hivi karibuni ya Marekani dhidi ya vituo na ngome za Jeshi la Iraq na makundi ya muqawama yanayopambana na ugaidi katika nchi hiyo ya Kiarabu.

Katika taarifa jana Jumatano, Yahya Rasoul, Msemaji wa Amiri Jeshi Mkuu wa Jeshi la Iraq alisema hujuma hizo za makombora za Marekani kaskazini mwa Iraq hazikubaliki na zimekiuka anga na mamlaka ya kujitawala nchi hiyo ya Kiarabu.

Rasoul amebainisha kuwa: Katika azma ya wazi ya kuvuruga usalama na uthabiti wa Iraq, Marekani imeendeleza mashambulizi yake ya anga dhidi ya vikosi vya jeshi la Iraq na harakati za kujitolea za wananchi (Hashdu Shaabi) katika maeneo ya Jurf al-Nasr na al-Qa’im, magharibi mwa Iraq."

Afisa huyo mwandamizi wa Jeshi la Iraq amesema Marekani imefanya mashambulizi hayo wakati huu ambapo eneo hili tayari linakabiliwa hatari ya kupanuka mgogoro uliosababishwa na vita vya Israel dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza. 

Haya yanajiri siku chache baada ya vikosi vya muqawama vya Iraq kukishambulia kwa maroketi na makombora 40 kituo cha wanajeshi vamizi wa Marekani cha A'inul-Assad kilichoko katika mkoa wa Al-Anbar, magharibi mwa Iraq.

Kufuatia mashambulio ya kinyama na jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina hususan wa Ukanda wa Gaza na uungaji mkono wa Washington kwa mashambulizi hayo, makundi ya muqawama ya Iraq yameionya Marekani kwamba yataendele kuvishambulia vituo vya nchi hiyo katika eneo.

Kambi na vituo vya muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Marekani katika nchi za Syria na Iraq vimeshambuliwa mara zaidi ya 130, tangu vilipoanza vita vya Gaza mnamo Oktoba 7 mwaka uliopita.

Tags