Jumuiya ya Nchi za Kiarabu yapinga vikali kuvunjwa UNRWA
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu amepinga mpango wowote wa kuvunjwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada na Ajira kwa Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) akisema hatua hiyo ni makosa ya kimaadili na kiusalama.
Ahmed Aboul Gheit amesema kuwa jaribio la baadhi ya nchi la kutaka kuivunja UNRWA kwa kusimamisha misaada yao ya kifedha kwa shirika hilo la Umoja wa Mataifa ni msimamo potofu kwa mtazamo wa kibinadamu na kimaadili, na pia ni makosa kwa mtazamo wa kiusalama.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ameongeza kuwa, mitazamo hatari likiwemo suala la kuvunjwa UNRWA inawakilisha matakwa ya kundi la mrengo wa kulia kupita kiasi la Israel ukiwa ni utangulizi wa kuwasahaulisha walimwengu suala la wakimbizi wa Kipalestina na kukomesha wajibu wa jamii ya kimataifa kwa taifa hilo.
Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu amepongeza misimamo ya Joseph Borrell, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, na nchi ambazo zimekataa wito wa kuharibiwa kwa makusudi shirika la UNRWA, haswa msaada wa Uhispania na Ureno kwa shirika hili, pamoja na upinzani wa Norway na Ireland dhidi ya kukatwa misaada ya shirika hilo la kutoa msaada ya kibinadamu.

Ahmed Aboul Gheit amesema kuwa watoto 250,000 wanasoma katika shule za UNRWA na zaidi ya Wapalestina 900,000 katika Ukanda wa Gaza wanapokea msaada wa chakula wa wa shirika hilo la UN.
Siku chache zilizopita maripota wa Umoja wa Mataifa walitangaza kwamba wanalaani vikali jaribio lolote la kuchafua sura ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada na Ajira kwa Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA).
Taarifa iliyotolewa na maripota wa UN kuhusiana na kusitishwa misaada ya kifedha ya baadhi ya nchi kwa shirika la UNRWA imesema: Nchi hizo zimechukua uamuzi huo baada ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) kufikia "uamuzi wa kimantiki" kuhusiana na mauaji ya kimbari ya Israel dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza.
Wakati huo huo, Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada na Ajira kwa Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA), Philippe Lazzarini amesema kwamba Israel bado haijatoa ushahidi wowote wa madai kwamba wafanyakazi kadhaa wa UNRWA waliohusika katika Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa Oktoba 7 mwaka jana.
Baadhi ya nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani zimekata misaada yao kwa shirika hilo la UN kutokana na madai yasiyo na msingi yaliyotolewa na utawala katili wa Israel.