Waziri Mkuu wa Serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina ajiuzulu
Waziri Mkuu wa Serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina Mohammad Ashtiyah, amejiuzulu wadhifa wake huo.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina, amekubali uamuzi wa kujiuzulu waziri mkuu wake huyo baada ya mashinikizo ya "nchi za eneo, jamii ya kimataifa, na hasa Marekani" kwa ajili ya kulifanyia mabadiliko baraza lake la mawaziri.

Inasemekana kuwa, mabadiliko ya Baraza la Mawaziri la Serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina yanafanywa kwa kisingizio cha kusimamisha vita katika Ukanda wa Ghazza, kutolewa hakikisho la kimataifa la kuondolewa kikamilifu majeshi ya utawala ghasibu wa Israel, kukomesha mashambulio yake katika ukanda huo na Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu pamoja na kuondolewa mzingiro wa kifedha waliowekewa Wapalestina.
Muhammad Mustafa, mkuu wa Mfuko wa Uwekezaji wa Palestina, ametajwa kuwa na nafasi kubwa zaidi ya kushika wadhifa wa Waziri Mkuu mpya wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina.
Kulingana na duru rasmi katika Mamlaka ya Ndani ya Palestina, serikali mpya itakayojumuisha mateknokrati huenda ikaundwa huko mjini Ramallah hadi ifikapo mwishoni mwa wiki hii.../