Syria: Kuunga mkono jinai za Netanyahu kumefichua dhati ya Wamagharibi
(last modified Mon, 11 Mar 2024 11:23:20 GMT )
Mar 11, 2024 11:23 UTC
  • Syria: Kuunga mkono jinai za Netanyahu kumefichua dhati ya Wamagharibi

Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria amezikosoa vikali nchi za Magharibi kwa kuendelea kuunga mkono jinai za kivita zinazofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza na kusisitiza kuwa, uungaji mkono huo umefichua dhati halisi ya Wamagharibi.

Faisal Mekdad amesema hayo katika ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa X na kuongeza kuwa, mauaji ya maelfu ya Wapalestina wakiwemo watoto 12,000 yamefichua undumukuwili wa Wamagharibi, ambao wamekuwa wakipiga nara hewa za eti kutetea haki za binadamu duniani.

Waziri Mekdad ameeleza bayana kuwa, "(Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin) Netanyahu ameugeuza Ukanda wa Gaza kuwa magofu, na kusababisha vifo vya watoto zaidi ya 12,000 na wanawake zaidi ya 8,000 Gaza."

Mekdad amesema hatua ya Israel ya kuendelea kufanya mauaji ya kutisha dhidi ya Wapalestina kwa uungaji mkono usio na kifani wa Magharibi imedhihirisha wazi dhati halisi ya kigaidi ya utawala huo na undumakuwili wa nchi za Magharibi.

Idadi ya Wapalestina waliouawa shahidi kufuatia mashambulio ya kinyama ya Israel katika Ukanda wa Gaza tokea Oktoba 7, 2023 mpaka sasa imekaribia 32,000.

Watoto wadogo, wahanga wakuu wa jinai za Israel huku Gaza

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Syria amesema kaulimbiu ambayo imekuwa ikipigiwa debe kwa muda mrefu na wanastratejia wa Umoja wa Ulaya ya kutaka kuwepo na nidhamu ya kimataifa yenye kuzingatia misingi ya sheria, haina maana tena.

"Kinachotisha zaidi ya jinai za Netanyahu na wenzake, ni uungaji mkono anaoupokea kutoka kwa serikali nyingi za EU, bila kusahau msaada na uungaji mkono pofu wa Washington (kwa jinai za Israel)," ameongeza mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Syria.