Waarabu wazipongeza nchi za Ulaya zilizolitambua taifa la Palestina
Mataifa ya Kiarabu yamekaribisha hatua ya baadhi ya nchi za Ulaya ya kutangaza rasmi kulitambua taifa la Palestina.
Katika taarifa zilizotolewa leo Alkhamisi katika nyakati tofauti, Wizara za Mambo ya Nje za Iraq, Kuwait na Saudi Arabia zimepongeza hatua hiyo ya nchi tatu za Ulaya ya kulitambua rasmi taifa la Palestina.
Zimesema hatua hiyo ya kutambuliwa Palestina mji mkuu wake ukiwa Quds itakuwa na mchango mkubwa wa kupatikana uthabiti katika eneo la Asia Magharibi, mbali na kuwadhaminia Wapalestina haki zao za msingi.
Aidha Misri na Qatar zilitangaza jana Jumatano kukaribisha uamuzi huo wa baadhi ya mataifa ya Ulaya kuitambua Palestina kama nchi huru. Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) pia imekaribisha uamuzi huo na kusema: Hatua hiyo ni muhimu katika mkondo wa sisi kudhaminiwa haki zetu kwa ardhi yetu.
Wakati huo huo, Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arabu League) imeutaka uamuzi huo kuwa wa kijasiri na ambao unaziweka nchi hizo tatu za Ulaya katika upande sahihi wa historia. Jana Jumatano, Ireland, Norway na Uhispania zilitangaza kulitambua rasmi taifa la Palestina, jambo ambalo limeukasirisha sana utawala haramu wa Israel.
Kadhalika nchi nyingine wanachama wa EU ambazo karibuni zlilitangaza kulitambua taifa huru la Palestina ni Slovenia, na Malta. Aidha siku chache zilizopita, Bahamas ilitangaza rasmi kuwa inaitambua rasmi Palestina kama nchi.
Nchi nyingine iliyounga mkono kutambuliwa kwa taifa la Palestina katika wiki za hivi karibuni ni "Trinidad na Tobago" inayopatikana katika Bahari ya Caribbean huko kaskazini mwa Amerika ya Kusini. Aidha mwezi uliopita, Jamaica na Barbados pia zilitangaza kuwa zinalitambua taifa la Palestina.